Wanawake wa Kimasai wanaopinga suala la tohara kwa
watoto wamegundua njia nyingine ya kukabiliana na ukeketaji kwa kutumia kupe
wakubwa.
Hayo
yalielezwa katika warsha ya kujipanga kupokea mradi wa kijiji cha dijitali,
iliyofanyika katika kijiji cha Ololosokwan hivi karibuni.
Wakijadili
changamoto ya ukeketaji kama sehemu ya shida kubwa ya jamii kiafya, wanawake
wamesema kwamba hukamata kupe wakubwa na kuwaua kisha kupiga vigelegele
kuonesha kwamba mabinti wao wamepewa tohara.
Mmoja
wa washiriki wa warsha hiyo alipouliza inakuwaje hapo baadaye binti
anapokuwa mkubwa, aliambiwa kwamba ni rahisi kwa binti huyo hapo baadae
kuzungumza na mwenzake wakaelewana.
“Tatizo
la tohara ni la wanaume, wanaume hawa ndio wanahimiza wanawake wawe na tohara
kwa kuwa wanataka kuwaoa wanawake ambao wameingia tohara kama wao,” alisema
mama mmoja.
Alisema
namna hiyo imefanya kuwakwepesha mabinti wengi na vurugu za tohara, ambazo
kiafya si sawa, hasa kutokana na tatizo linaloambatana na kovu wakati wa uzazi
na pia kwenye uhusiano wa kimapenzi kwa upande wa mwanamke.
Katika
warsha hiyo, ambapo pia suala la ndoa za utotoni na mimba za utotoni
zilijadiliwa, ilielezwa kuwa elimu
inatakiwa kupewa watu wa mila ili kutambua athari za mimba na ndoa za utotoni.
Kijiji
cha dijitali cha Ololosokwan, kinatarajiwa kuwa na huduma zote za kijiji
cha kisasa kama umeme, afya na kituo cha utamaduni, ambacho kitaunganisha
watalii na wananchi ili kuwawezesha kiuchumi.
No comments:
Post a Comment