Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za
Nishati na Maji (EWURA), imetangaza kushuka zaidi kwa bei za bidhaa za mafuta
hapa nchini kuanzia leo, kutokana na bei katika soko la dunia kuendelea
kuporomoka.
Mwezi uliopita, kwa mara ya kwanza
baada ya muda mrefu, bei ya petroli, dizeli na mafuta ya taa ilishuka kwa kiasi
kikubwa, mathalani bei ikifikia chini ya Sh 2,000. Na jana, bei ya juu kabisa
ya petroli ilitangazwa kushuka kwa Sh 187 zaidi.
Nafuu hiyo ya bei ilitangazwa na
Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Felix Ngamlagosi, akisema bei hizo za kikomo za
bidhaa ya mafuta zitaanza kutumika leo nchi nzima na kwamba mabadiliko hayo ya
bei yanatoka na kushuka kwa bidhaa hiyo katika soko la dunia.
Alisema bei za jumla na rejareja kwa
aina zote za mafuta yakiwemo petroli, dizeli na mafuta ya taa zimeshuka,
ikilinganishwa na bei katika toleo lililopita la Januari 7, mwaka huu.
“Katika toleo hili bei za rejareja kwa
petroli zimepungua kwa Sh 187 kwa lita sawa na asilimia 9.56, dizeli imepungua
kwa Sh 139 kwa lita sawa na asilimia 7.53 na mafuta ya taa yamepungua kwa Sh
177 kwa lita sawa na asilimia 9.64,” alisema.
Aidha, alisema kwa kulinganisha matoleo
hayo mawili bei za jumla zimepungua ambapo petroli imepungua kwa Sh 186.89 kwa
lita sawa na asilimia 10.08, dizeli Sh 138.97 kwa lita sawa na asilimia 7.97 na
mafuta ya taa kwa Sh 176.64 kwa lita sawa na asilimia 10.20.
“Bei za mafuta masafi katika soko la
dunia kwa petroli, dizeli na mafuta ya taa zimepungua kati ya mwezi Julai na
Desemba 2014 kwa takribani dola 440 kwa tani, dola 304 kwa tani na dola 324 kwa
tani sawia sawa na punguzo la asilimia 44,35 na 35 sawia,” alisema.
Alisema kati ya mwezi Septemba 2014 na
Februari 2015, bei za petroli, dizeli na mafuta ya taa katika soko la ndani
zimepungua kwa Sh 499 kwa lita, Sh 384 kwa lita na Sh 384 kwa lita sawia,
ambayo ni sawa na punguzo la asilimia 22, 18 na 19 sawia.
"Katika kipindi husika, thamani ya
shilingi ya Tanzania ikilinganishwa na dola ya Marekani imeshuka kwa asilimia
6. Bei ya mafuta kwenye soko la ndani ingeweza kupungua zaidi kama thamani ya
shilingi isingeendelea kudhoofu," alisema.
Pia, Ngamlagosi alisema ni muhimu
kuzingatia kwamba kwa wastani bei za mafuta katika soko la dunia na gharama za
uagizaji (CIF) huchangia asilimia 60 ya bei ya mafuta katika soko la ndani, hivyo
kiwango cha ushukaji bei katika soko la ndani hakiwezi kuwa sambamba na
asilimia ya ushukaji katika soko la dunia.
"Kampuni za mafuta zipo huru kuuza
bidhaa za mafuta ya petroli kwa bei ya ushindani ilimradi bei hizo ziko chini
ya bei ya kikomo kama ilivyokokotolewa na fomula iliyopitishwa na EWURA na
ambayo ilichapwa kwenye gazeti la serikali namba 354 la Septemba 26,
2014," alisema.
Alisema vituo vyote vya mafuta
vinatakiwa kuchapisha bei za bidhaa za mafuta katika mabango yanayoonekana
bayana na yakionesha bei ya mafuta, punguzo, vivutio vya biashara au promosheni
zinazotolewa na kituo husika.
"Pale ambapo inawezekana kuchagua
wateja wanashauriwa kununua bidhaa za mafuta kutoka kwenye vituo vinavyouza
mafuta kwa bei ndogo zaidi ili kuimarisha ushindani. Ni kosa kuuza mafuta bila
kuweka mabango ya bei inayoonekana vizuri kwa wateja na adhabu itatolewa kwa
kituo husika," alisema.
Aidha aliwataka wanunuzi kuhakikisha
wanapata stakabadhi ya malipo inayoonesha jina la kituo, tarehe, aina ya mafuta
yaliyonunuliwa na bei kwa lita.
Alisema stakabadhi hiyo ya malipo
itatumika kama kidhibiti cha mnunuzi wa mafuta endapo kutajitokeza malalamiko
ya ama kuuziwa mafuta kwa bei ya juu kuliko bei kikomo au endapo mnunuzi
atakuwa ameuziwa mafuta yenye kiwango cha ubora kisichofaa.
Alisema bei za kikomo kwa Dar es Salaam
bei za rejareja kwa lita moja ya petroli ni Sh 1,768, dizeli Sh 1,708 kwa lita na mafuta ya taa ni
Sh 1,657 kwa lita huku bei za jumla ikiwa ni Sh 1,666.43 kwa lita ya petroli,
Sh 1,605.52 kwa lita ya dizeli na Sh 1,554.59 kwa lita ya mafuta ya taa.
Hata hivyo, alizitaka mamlaka
mbalimbali kuhakikisha zinawawezesha wananchi kuona manufaa ya kupungua kwa bei
ya bidhaa hiyo hasa katika sekta ya usafirishaji na nishati ya umeme.
Pamoja na nafuu hiyo ya bei, wataalamu
mbalimbali wa masuala ya uchumi, wakiwemo wanasiasa waliohoji kwa muda mrefu
sababu za kutoshuka kwa bei ya mafuta nchini, hawakuwa tayari kuzungumzia
mapema juu ya punguzo hilo la bei.
Zitto Kabwe, Mchumi na Mbunge wa Kigoma
Kaskazini anayeiongoza Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC),
alipotafutwa kuzungumzia hilo, alisema hajapata taarifa rasmi, hivyo hatakuwa
tayari kusema lolote.
Hata hivyo, shauku ya Watanzania wengi
ni kuona kwamba, gharama za maisha, zikiwemo za usafiri na usafirishaji
zinazoumiza wengi kwa kile kinachodaiwa kupanda kwa gharama za vipuri na hata
nishati ya mafuta.
No comments:
Post a Comment