BUNGE LAMSHAMBULIA DPP KUKWAMISHA JUHUDI ZA TAKUKURU


Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka Nchini (DPP) imetajwa kudhoofisha juhudi za Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), kutokana na ama kuchelewesha au kutokutoa vibali vya kufikisha mahakamani kesi kwa makosa makubwa ya rushwa.

Bunge limeambiwa kwamba gharama nyingi za serikali, zimekuwa zikitumika katika kufanya uchunguzi wa tuhuma za rushwa, lakini majalada yanapowasilishwa kwa DPP, mengi hayatolewi vibali na huachwa kwa kigezo cha kutokuwa na ushahidi wa kutosha, jambo linalosababishia serikali hasara.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala, kupitia kwa Mwenyekiti wake, Jasson Rweikiza ilisema hayo jana wakati wa kuwasilisha taarifa ya mwaka ya shughuli zake kuanzia Januari, 2014 hadi Januari mwaka huu.
Rweikiza, ambaye alizungumzia maeneo mbalimbali ambayo kamati yake ilifanyia kazi, alisema pamoja na upungufu wa fedha unaokabili Takukuru, ulazima wa kupata kibali kutoka kwa DPP ni changamoto nyingine.
“Jambo hili limekuwa likidhoofisha juhudi zake katika mapambano ya rushwa kwani vibali huchelewa kutolewa na wakati mwingine havitolewi kabisa,” alisema mwenyekiti huyo wa kamati.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya kamati, katika kipindi cha kuanzia Julai mwaka jana hadi Januari mwaka huu, taasisi imechunguza majalada 3,014 ya rushwa na kati ya hayo, Takukuru imefungua kesi 108 mahakamani ambazo ni sawa na asilimia 3.8.
Kamati imeshauri serikali kuimarisha taasisi hiyo kwa kuipa mamlaka kamili ya kufungua mashitaka na kuyaendesha mahakamani bila kuomba kibali cha DPP.
Bunge lilielezwa kwamba Takukuru kwa sasa ina uwezo wa kutosha kujisimamia kwa kuwa na rasilimali watu na nyenzo za kazi, tofauti na ilivyokuwa awali ambapo shughuli za kufungua na kuendesha mashitaka mahakamani ilikasimiwa na Kurugenzi ya Mashitaka.
Aidha, kamati imependekeza, kutokana na kuongezeka kwa matukio ya rushwa nchini, kianzishwe chombo kingine kipya kitakachoshughulikia makosa madogo ya rushwa na kuachia Takukuru kushughulikia rushwa kubwa zenye athari kubwa za kiuchumi na kijamii.
Wakati huo huo, akizungumzia Idara ya Mahakama, Rweikiza katika taarifa hiyo ya kamati, alisema mhimili huo unakabiliwa na mmomonyoko wa maadili kwa baadhi ya watumishi ambao wanashughulikia utoaji haki. “Baadhi ya viashiria vya mmomonyoko huo ni pamoja na vitendo vya rushwa,” alisema.
Katika kuchangia, Mbunge wa Viti Maalumu, Diana Chilolo (CCM) alisema mahakimu wanafanya kazi katika mazingira magumu kutokana na uchache wao, hali ambayo hurundikiwa kesi.
Alishauri katika bajeti ijayo, wabunge wahakikishe inatengwa ya kutosha iwezeshe pia ujenzi wa mahakama za wilaya kwa nchi nzima.

No comments: