Wakurugenzi
21 katika Halmashauri mbalimbali nchini wamevuliwa madaraka katika
kipindi cha mwaka 2013 hadi 2015 huku 27 wakipewa onyo na sasa kesi zao zikiwa
mahakamani kwa tuhuma mbalimbali, ikiwemo matumizi mabaya ya fedha.
Aidha, wafanyakazi 233 wamefukuzwa kazi na mabaraza ya madiwani na
wengine 372 kesi ziko mahakamani huku 10 zikiwa zimetolewa uamuzi wa kufungwa
na wengine kutozwa faini.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Hawa Ghasia alisema hayo
wakati akijibu hoja za Kamati ya Kudumu
ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa
(LAAC) kuhusu madai ya kuhamisha watumishi wenye tuhuma bila kuwachukulia
hatua.
Ghasia alisema iwapo kuna watumishi waliohamishwa bila kujua na
inapofahamika wanarudishwa kituo cha kazi kujibu tuhuma kwani si sera ya wizara
yake kuwahamisha kwa makusudi watumishi wanaotuhumiwa kwa makosa mbalimbali wanawachukulia
hatua za kisheria.
Akizungumzia suala la miradi ya chini ya kiwango, alisema kuanzia mwaka
jana wamepitia muundo wao na kuunda idara ya ufuatiliaji na tathmini ya ubora
katika miradi ya halmashauri na ikiwa chini ya kiwango hatua zinachukuliwa
kabla Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) hajafika kukagua.
Katika suala la kuongeza mapato katika halmashauri, alisema mwaka 2013
walifanya utafiti wa kuainisha vyanzo vipya vya mapato na kupata ushuru wa minara ya simu, nyumba za kulala
wageni na halmashauri kutoza kodi yamajengo.
“Lakini pia tunatarajia kurekebisha sheria ya fedha katika serikali za mitaa na tayari
rasimu ya kwanza imekamilika kwa lengo
la kuongeza vyanzo vya mapato katika halmashauri,” alisema.
No comments:
Post a Comment