Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini,
imeitaka Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) kufanya
ukokotoaji upya wa bei ya mafuta ili kumsaidia mlaji wa mwisho wa bidhaa hiyo
kunufaika na punguzo la bei ya mafuta duniani.
Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa shughuli za kamati hiyo, Mbunge
wa Tandahimba, Juma Njwayo (CCM) kwa niaba ya mwenyekiti wa kamati hiyo alisema
utaratibu huo wa Ewura wa M-One wauangalie upya kwani unaumiza mlaji.
Alisema bei ya bidhaa hiyo duniani imeshuka kwa asilimia 60. Dar es
Salaam hutumia asilimia 60 ya mafuta yanayoagizwa nchini huku kampuni zinazouza
mafuta yanauza lita moja Sh 1,520 kwa jumla.
Njwayo alisema lakini katika vituo vya rejareja Dar es Salaam bidhaa
hiyo huuzwa Sh 1,849 tofauti ya Sh 329 kwa lita moja, kwani kutokana na kushuka kwa bei hiyo ya mafuta duniani inaweza kushuka kila mwezi.
Pia alisema kamati inashauri serikali kwa ushirikiano na wawekezaji
binafsi kuanza ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta kutoka Dar es Salaam
kwenda mikoani ili kupunguza gharama za mafuta, usalama wa usafirishaji pamoja
na usalama wa barabara nchini.
Kamati hiyo iliishauri serikali kuachana na mitambo ya kukodi ya kampuni
ya Songas-Gas, IPTL na Symbion kama ilivyofanya kwa Aggreko na kununua mitambo
yake ili kuliondolewa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) gharama kubwa ya
capacity charge kwani mitambo ya kukodi gharama yake ni kubwa.
Alisema Tanesco iweke mpango maalumu wa muda mfupi kati na mrefu kukusanya madeni yote wanayodai
watu binafsi, serikali na taasisi zake ambazo ni Sh bilioni 186.4 na kulipwa
moja kwa moja kupitia hazina.
Akizungumzia suala la sekta ndogo ya gesi, alisema kamati imeridhishwa
na hatua za kumalizia ujenzi wa bomba
gesi na miundombinu yote ifikapo Juni, mwaka huu.
“Hata hivyo, tunaomba serikali kuhakikisha Sera Mpya ya Gesi inawafikia
wananchi na wadau wengi huku uagizaji mafuta kwa pamoja ukipunguza kero nyingi
za upatikanaji wa mafuta na udhibiti wa bei ya bidhaa hiyo,” alisema Njwayo.
Aliitaka serikali kuandaa sera na sheria kuhusu masuala ya joto ardhi na
mchakato huo kushirikisha wadau kwa lengo la kuwa na vyanzo mbadala vya umeme
nafuu na endelevu nchini baada ya kuundwa kwa kampuni ya umma ya kusimamia
tafiti, uanzishaji na uendelezaji wa miradi hiyo.
No comments:
Post a Comment