MZEE JUMBE ATOA SHUKRANI ZAKE


Rais mstaafu wa Awamu ya Pili ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Alhaji Mzee Aboud Jumbe (95), ameishukuru Serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwa kumhudumia kwa hali na mali, sambamba na kuendelea kumjulia hali.

Mzee Jumbe alisema hayo jana jijini Dar es Salaam, alipotembelewa nyumbani kwake na viongozi wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, akiwemo Mkuu wa Mkoa huo, Said Meck Sadiki, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 38 ya chama hicho.
Akizungumza kwa shida huku akisaidiwa kufikisha ujumbe na Msaidizi Mkuu wake, Abuu Mbange, Mzee Jumbe alisema; “Nawashukuru sana kwa kuja kuniona Mwenyezi Mungu awajalie kila heri.” 
“Nawashukuru sana kwa kuja kwenu, hali yenyewe ndo kama mnavyoiona, miaka 95 sasa sioni, kusikia ni vigumu, sauti nayo inakimbia. Mwenyezi Mungu awajalie heri na Watanzania wote,” alisema Mzee Jumbe.
Alishukuru viongozi mbalimbali wanaojitokeza kumtembelea mara kwa mara, akiwemo Rais Jakaya Kikwete na kuwaombea Mungu awajalie afya njema pamoja na Watanzania wote.
Mbange, ambaye  amekuwa Msaidizi Mkuu wa Mzee Jumbe tangu alipokuwa Makamu wa Rais na Rais wa Zanzibar kwa takribani miaka 35 sasa,  alisema kiongozi huyo amekuwa akisumbuliwa na kichwa kwa muda mrefu, ingawa afya yake ni njema.
Alisema pamoja na tatizo hilo, lakini hali ya Mzee Jumbe ni njema na bado ana uwezo wa kuandika vitabu vikiwemo vya siasa na vya dini na anafanya uandishi wa vitabu kwa kutoa maagizo kwa wasaidizi wake, na mpaka sasa ameshaandika vitabu zaidi ya 30.
Kwa mujibu wa Mbange, kutokana na hali ya uzee ya kiongozi huyo, amejikuta akishindwa kutekeleza majukumu yake kama zamani na hivyo kutoa maagizo kwa wasaidizi wake wayafanyie kazi.
“Mzee Jumbe anasumbuliwa na uzee na utu uzima, lakini kiakili bado hali yake ni nzuri na amekuwa akiendelea kuandika vitabu vingi, vingi vikiwa vya dini tangu aache uongozi wa kitaifa. Vitabu hivyo amekuwa akiviandika kwa kutoa maelekezo kwa wasaidizi wake,” alisema.
Ataja baadhi ya vitabu alivyoviandika kuwa ni ‘Partnership’ na  Safarini ambavyo amekuwa akihamasisha waumini wa dini ya Kiislamu kumjua  Mtume wao.
“Kwa sasa Mzee Jumbe amekuwa akizungumzia zaidi historia ya Chama cha ASP, uongozi wa Mzee Abeid Amani Karume, uongozi wa Mwalimu Julius  Nyerere na pia kila mara amekuwa akitamani kuonana na viongozi mbalimbali ndani ya Serikali na chama kwa ajili ya kuwapa ya moyoni mwake,” alisema.
Wake wa Mzee Jumbe, Zeyana Rashid Mohamed na Fatma Mohamed Hassan, waliishukuru Serikali na Chama kuendelea kumkumbuka Mzee huyo na kusema kwamba hali yake si mbaya isipokuwa tatizo ni kichwa na wamekuwa wakienda India kila baada ya miezi muitatu kwa ajili ya uchunguzi.
Walisema tatizo hilo la kichwa lilikuwa likimsumbua tangu akiwa mdogo kwa hiyo siyo geni lakini tatizo kubwa ni uzee.
Zeyana aliwaomba Watanzania wakisherehekea miaka 38 ya CCM, kuendelea kumuombea Mzee Jumbe afya njema na kuzidi kumtembelea.
"Kama mnavyoona hali yake ya uzee ndio inamfanya awe hivyo kwa sababu uzee hauna dawa... si mnamuona amelala tu na ndiyo maana tumewaomba hata msimpige picha," alisema.
Mzee Jumbe ana wake wanne lakini wawili walifariki na watoto 17 ambao wanne wameshatangulia mbele ya haki.

No comments: