EATV REDIO, TELEVISHENI KUTOA ELIMU YA UCHAGUZI


Kituo cha Televisheni  cha EATV na kituo chake cha East Africa Radio wameandaa kampeni maalumu itakayojulikana kama Zamu yako 2015 kwa ajili ya kuwakumbusha na kuwaelimisha vijana umuhimu pamoja na uwezo walionao katika kufanya maamuzi sahihi kwenye masuala makubwa ya kitaifa yanayohusu siasa.

Akizungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Mkuu wa Vipindi wa EATV Radio na Televisheni, Nasser Kingu, alisema kampeni hiyo imeshaanza na dhamira yake ni kuwahimiza vijana kutumia fursa waliyonayo katika kufanya maamuzi katika mambo makuu matatu.
Alisema mambo hayo ni kuwahimiza vijana kushiriki kikamilifu katika uandikishaji kwenye daftari la kudumu la wapiga kura, kisha kushiriki kikamilifu katika  kupiga kura ya maoni katika mchakato wa kutafuta Katiba mpya na kushiriki kikamilifu katika suala la upigaji kura ili kuchagua viongozi wanaowataka.
“Hatma ya taifa hii iko mikononi mwa vijana na ndio maana kituo chetu kimeamua kuchukua jukumu la kuendesha kampeni hii kwa kutambua umuhimu na nguvu ya vijana katika Taifa letu,” alisema Kingu.
Pia alisema katika kampeni hiyo vijana watapatiwa elimu ili kujua umuhimu wa kupiga kura ili waweze kufanya maamuzi sahihi katika uchaguzi baada ya kupatiwa elimu hiyo.
Aliongeza kuwa njia zitakazotumika kufikisha elimu hiyo kwa wananchi ni vipindi katika redio na televisheni, mahojiano na wageni na matangazo na elimu itafika katika  mikoa 15 ambayo redio inasikika, pamoja na mitandao ya kijamii.

No comments: