Mahakama
ya Hakimu Mkazi Kisutu imepanga Februari 18, mwaka huu kusikiliza ombi la
kwenda kutibiwa nchini India, lililowasilishwa na mshitakiwa wa kesi ya wizi wa
Sh milioni 207 katika Benki Kuu (BoT) kupitia Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA)
Rajab Maranda.
Kesi
hiyo ilitajwa kwa ajili ya kusikiliza ombi hilo lakini Hakimu Mkazi Frank
Moshi, aliahirisha kwa kuwa jopo la mahakimu wanaosikiliza kesi hiyo
halikukamilika.
Awali
Wakili wa Serikali, Shadrack Kimaro alidai kesi imetajwa kwa ajili ya
kusikiliza ombi la Maranda (pichani) lakini aliomba Mahakama ipange tarehe nyingine ya
kutajwa kwa kuwa jopo linalosikiliza kesi halikufika.
Aidha
upande wa utetezi uliomba Mahakama itoe kibali kwa mshitakiwa Farijala Hussein
kupewa kibali cha kusafiri. Hakimu Moshi alisema hawezi kutoa kibali hicho na
kuwashauri wawasilishe ombi hilo mbele ya jopo la mahakimu linalosikiliza kesi
hiyo.
Washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Imani Mwakosya,
Esther Komu na Bosco Kimela. Wanakabiliwa na mashitaka ya kuwasilisha nyaraka
za uongo, kughushi, kuiba Sh milioni 207 kutoka BoT na kusababisha hasara ya
fedha hizo.
Inadaiwa kuwa washitakiwa walighushi nyaraka, ambazo ni
pamoja na hati za makubaliano ya kuhamishiwa deni kutoka Kampuni ya General
Marketing ya India kwenda Kampuni ya Rashaz (T) ya Tanzania, ambazo walizitumia
na kuiba fedha hizo.
No comments:
Post a Comment