WIMBI LA ESCROW LASOMBA VIGOGO WENGINE WATATU


Vigogo wengine watatu wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashitaka ya kupokea rushwa ya zaidi ya Sh bilioni 2.4 ambazo ni sehemu ya fedha zilizokuwa kwenye akaunti ya Tegeta Escrow.

Washitakiwa hao ni Meneja Misamaha ya Kodi TRA, Kyabukoba Leonard Mutabingwa, Mwanasheria Mwandamizi wa Shirika la Umeme(Tanesco),  Steven Urassa na Mkurugenzi wa Fedha Benki Kuu (BoT), Julius  Angello.
Washitakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo jana na kusomewa mashitaka na Wakili kutoka  Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Leonard Swai mbele ya mahakimu wawili tofauti.
Katika kesi inayomkabili Kyabukoba, Wakili  Swai   alidai mbele ya Hakimu Mkazi Janeth Kaluyenda kuwa Januari 27,2014 katika benki ya Mkombozi  wilaya ya Ilala , alipokea Sh 1.6 bilioni kutoka kwa Mkurugenzi wa kampuni ya kufua umeme ya VIP ambaye alikuwa Mkurugenzi wa IPTL James Rugemalira.
Swai alidai Kyabukoba alipokea fedha hizo kupitia akaunti namba 00110202613801 ambazo ni sehemu ya fedha zilizokuwa kwenye akaunti ya Tegeta Escrow  kama tuzo kwa kuiwakilisha kampuni ya  Mabibo Beer Wines and Spirits ambayo ni mali  ya Rugemalira  mahakamani,  kitu ambacho ni kinyume cha sheria.
Aidha anadaiwa Julai 15,2015, Kyabukoba  akiwa  katika benki hiyo alipokea rushwa ya Sh milioni 161.7 , Agosti 26,2014 alipokea tena rushwa ya Sh milioni 161.7 na  Novemba 14,2014 alijipatia rushwa Sh milioni 161.7 kupitia kwenye akaunti hiyo, kama tuzo kwa kuiwakilisha kampuni hiyo ya  Rugemalira mahakamani.
Inadaiwa fedha zote hizo ni sehemu ya fedha zilizokuwa kwenye akaunti ya Tegeta Escrow. Katika kesi inayomkabili  Angello mbele ya Hakimu Mkazi, Devotha Kisoka, Wakili Swai alidai Februari 6, 2014 katika benki hiyo ya Mkombozi alipokea rushwa ya Sh milioni 161.7 kutoka kwa Rugemalira kupitia akaunti namba 00120102646201.
Swai alidai Angello alipokea fedha  hizo ambazo ni sehemu ya fedha za akaunti ya Tegeta Escrow kama tuzo kwa kuisaidia katika malipo yaliyotolewa katika Akaunti ya Tegeta Escrow, kwa kampuni ya PAP kulipwa jambo ambalo lilikuwa ni kinyume na mwajiri wake.
Kwa upande wake Mwanasheria Mwandamizi wa Tanesco,  Urassa , anadaiwa Februari 14,2014 akiwa katika benki hiyo alipokea rushwa ya Sh milioni 161.7 ambazo ni sehemu ya fedha zilizokuwa kwenye akaunti ya Tegeta Escrow.
Wakili Swai alidai, Urassa alipokea fedha hizo kupitia akaunti  namba 00120102658101  kutoka kwa Rugemalira kama tuzo kwa kuiwakilisha mahakamani Tanesco na kampuni nyingine zilizoingia nazo mkataba. Washitakiwa wote walikana mashitaka na upande wa Jamhuri ulidai upelelezi wa kesi hizo umekamilika na kuomba tarehe nyingine ya kuwasomea washitakiwa maelezo ya awali.
Aidha Mahakama imeamuru akaunti zote za washitakiwa zilizo na fedha zinazobishaniwa mahakamani zisitumike hadi kesi za msingi zitakapokwisha. Kyabukoba alirudishwa rumande baada ya kushindwa kutimiza masharti ya kuwa na wadhamini watatu wa kuaminika, watakaosaini hati ya dhamana ya Sh milioni 340.
Aidha alitakiwa atoe fedha taslimu Sh bilioni moja ambayo ni nusu ya fedha anazodaiwa kupokea au kuwasilisha hati ya mali isiyohamishika yenye thamani ya fedha hizo, pia asitoke nje ya mkoa bila kibali cha Mahakama. Angello aliachiwa kwa dhamana baada ya kukamilisha masharti ya kutoa fedha taslimu Sh milioni 80.8 au kuwasilisha hati ya mali isiyohamishika yenye thamani hiyo,  awe na wadhamini wawili wanaominika, mmoja kati yao awe mtumishi wa serikali  na kila mdhamini asaini hati ya Sh milioni 50. Kesi itatajwa Januari 27. 
Urassa aliachiwa kwa dhamana baada ya kuwa na wadhamini  wawili wanaoaminika  na kuwasilisha mahakamani hati ya mali isiyohamishika yenye thamani Sh milioni  81.

No comments: