WENYE SHAHADA YA CPA SASA WAFIKIA 6,002


Jumla ya watahiniwa 356 wamefaulu mtihani wa shahada ya juu ya uhasibu nchini (CPA) na kufanya watahiniwa waliofaulu mitihani hiyo  kufikia 6,002 tangu mitihani hiyo ilipoanza mwaka 1975.

Matokeo hayo yameidhinishwa katika kikao cha tatu maalum cha Wakurugenzi wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu(NBAA) kilichokaa Januari 15.
Mkurugenzi Mtendaji wa NBAA, Pius Maneno alisema kuwa kati ya watahiniwa hao wanawake ni 95 sawa na asilimia 26.7 na wanaume ni 261 sawa na asilimia 73.3.
Alisema katika matokeo ya jumla watahiniwa waliosajiliwa walikuwa 6,464 kati ya hao watahiniwa 678 sawa na asilimia 10.5 hawakuweza kufanya mitihani hiyo kwa sababu mbalimbali hivyo watahiniwa waliofanya mitihani walikuwa 5,786.
Alisema kati ya watahiniwa hao watahiniwa 1,260 ambao ni asilimia 21.8 wamefaulu mitihani yao katika ngazi husika, watahiniwa 1,811 ambao ni sawa na asilimia 31.3 wamefaulu baadhi ya masomo katika ngazi husika na watahiniwa 2,715 ambao ni asilimia 46.9 hawakufaulu mitihani hiyo.
Alisema kwa upande wa cheti cha utunzaji wa hesabu (ATEC) watahiniwa 43 wamefaulu  na hivyo kufanya idadi ya watahiniwa waliofaulu mitihani ya cheti kufikia 3,523 tangu mitihani hiyo ianze mwaka 1991.

No comments: