Viongozi wa dini za Kiislamu na Kikristo nchini
wamekubaliana kutoandaa mihadhara inayokashifu dini moja na nyingine, miongoni
mwa madhehebu ya dini moja au kashfa baina ya waumini na waumini.
Lengo la makubaliano hayo ni kudhibiti madhara ya mihadhara hiyo ambayo
imeonekana inachangia uchochezi wa ugaidi na uvunjifu wa amani.
Katibu Mkuu wa Taasisi ya Mashehe na Wanazuoni wa Kiislamu
Tanzania, Shehe Hamis Mataka aliyasema
hayo jana Dar es Salaam, wakati
akifungua kongamano la siku mbili lililoandaliwa na Iman Burkhary Islamic
Foundation, linalojadili madhara ya misimamo mikali ya imani za dini.
Shehe Mataka alisema kwamba viongozi wa dini zote wasimame imara kukemea
watu wanaojitokeza kuchochea uvunjifu wa amani kupitia dini.
Alisema kwamba wapo watu wanaotumia dini kujipatia maslahi yao binafsi,
badala ya kuwafundisha watu kufuata mafundisho sahihi ya Mungu kwa kuhimizana
upendo na amani.
‘’Kongamano hilo limekuja wakati sahihi kuangazia yaliyo ndani ya nchi
yetu. Sisi Waislamu hatuna tatizo na Wakristo nao vivyo hivyo hawana tatizo na
sisi kwa sababu sote tunatambua uwepo wa dini zote,’’alisema Shehe Mataka.
Alisema kuwa mafunzo yasiyo sahihi na upotoshwaji wa dini unaofanywa na
baadhi ya watu unatakiwa kukemewa kwa nguvu zote ili uovu utokanao na
upotoshwaji huo usije kuiangamiza nchi.
Aliongeza kuwa endapo hakutakuwa na mihadhara inayochochea hasira na
uvunjifu wa amani nchini, viongozi hao wa dini wataweza kuwakemea viongozi
waliopo serikalini watakaokiuka maadili.
“Ikigundulika mtu anasimama na kupotosha mafundisho ya dini ni lazima
tusimame kidete kumkataa mtu huyo kwani hafai kwa kuwa anachochea mauaji,”
alisisitiza.
Kwa upande wake, Askofu wa Kanisa la Galilaya Temple lililopo Msasani,
Dk Philbert Mbepera aliwaasa viongozi wenzake kutobeza dini hata kama mtu
ataonekana kuuabudu mti.
Dk Mbepera alisema amani ya nchi hii haiwezi kujengwa na watu wengine
bali kwa kuhamasishana upendo na kuvumiliana.
Alisema waumini wasilazimishane kuamini dini fulani bali kuelekezana na
kuonyana wanapokosea. Pia alisema wameanza kufanya maombi ya siku 40 kuombea
amani ya nchi kwani bila ya kufanya hivyo madhara makubwa yanaweza kutokea.
Hata hivyo, Shehe wa Masjid ya Qhadir Kigogo Post, Hemed Jalala alisema
kwamba viongozi wa dini watasaidia katika kuwaelimisha vijana juu ya madhara ya
ugaidi na ukatili.
Alisema endapo vijana hao wataendekeza ugaidi ambao unainyemelea nchi, hawatakuwa salama na watavuruga amani ya nchi.
“Madhumuni ya kuwaleta Waislamu na Wakristo katika kongamano hili ni
kutathmini matokeo endapo fikra za ugaidi zitakapoingia nchini. Tumpige vita
mdudu huyu mbaya asije akaingia tukashindwa kupata muda wa kumuabudu Mungu, ’’
alisema Shehe Jalala.
Alisema endapo vijana hao wataendekeza ugaidi ambao unainyemelea nchi, hawatakuwa salama na watavuruga amani ya nchi.
Aliwaasa vijana kuvumiliana katika kila hali na kwamba wanasiasa
watakaokwenda kombo watawekwa chini na kukemewa.
No comments:
Post a Comment