Wakazi watano wa kitongoji cha Mafuriko Amboni
kilichopo jijini Tanga wamejeruhiwa vibaya sehemu mbalimbali za mwili baada ya
kurushiwa bomu la kutupwa kwa mkono na
mtu asiyejulikana wakati walipokuwa wakitazama mpira kwenye banda la wazi.
Majeruhi hao ni Hassani Abdallah (72) ambaye amevunjika mguu wa kulia na
kupata madhara makubwa kifuani na sasa amelazwa katika hospitali ya mkoa ya
Bombo. Wengine ni Rashid Ally (45), Mrisho Abdi (29), Juma Mtoo (15) na Abdul Ismail
(19) ambao waliumia sehemu mbalimbali za mwili lakini baada ya kufikishwa Bombo
wamepatiwa matibabu na kuruhusiwa kurudi nyumbani.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Tanga, Frasser Kashai amethibitisha tukio hilo
na kusema limetokea Januari 15 mwaka huu saa 3:00 usiku huko Mafuriko wakati
waathirika hao walipokuwa ndani ya banda moja la kuonesha video.
“Ni kweli jana usiku huko Amboni Mafuriko katika kata ya Chumbageni
kulitokea mlipuko wa kitu kinachodhaniwa kuwa ni bomu”, alisema.
Aidha aliongeza, “Bomu hilo lilirushwa majira ya saa 3:00 usiku kwenye
banda la wazi la kuonyesha video ambalo ni mali ya Evarist Kingazi (82) na
kusababisha majeruhi watano”, alisema.
Alisema uchunguzi wao wa awali umebaini kwamba bomu hilo ni la
kutengenezwa kienyeji kwa sababu askari waliofika eneo la tukio walifanikiwa
kuokota mabaki yake ambayo yamejumuisha vipande kadhaa vya nondo na vibati
vidogo vidogo. Kamanda Kashai alisema mkazi mmoja wa eneo hilo, Ally Rashid
(25) anashikiliwa na Polisi kwa mahojiano maalumu kuhusiana na tukio hilo.
No comments:
Post a Comment