MKE NA MUME MBARONI KWA MAUAJI YA MGANGA WA JADI

Jeshi la Polisi mkoani Kagera linawashikilia watu tisa kwa tuhuma za mauaji  katika matukio mawili tofauti wakiwemo mume na mke waliomuua mganga wa jadi.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi mkoani hapa Henry Mwaibambe, alisema tukio la kwanza lilitokea saa 3:00 usiku wa Januari 14 mwaka huu katika kata ya Bugarama wilayani Ngara ambapo mganga wa jadi, Alfaxad John ( 36 ) akiwa anaendesha pikipiki yake yenye namba za usajili T.237 CDK  alikufa baada ya kupigwa na  kitu chenye ncha kali.
Alisema inaaminika mganga huyo alipigwa na shoka kichwani  na kusababisha kichwa kugawanyika sehemu mbili  na shingo kutenganishwa.
Alisema siku mbili kabla ya tukio hilo la mauaji John aliibiwa mbuzi watano nyumbani kwake, aliwaona wezi  lakini hakutoka nje ili kulinda usalama wake. Baada ya muda alipata ujumbe  wa simu ya mkononi kutoka  kwa  mpenzi wake ukisema “pole mpenzi  nipo  pamoja na wewe  ungetoka nje ili kukabiliana na wezi hao ungeuawa”.
Aliwataja watuhumiwa wanaoshikiliwa kuwa ni Burhani Tutuleka (40 ) mwalimu wa shule ya msingi Rwinyana iliyoko kata ya Bugarama na mkewe Madina Khamisi (35).
Ingawa chanzo cha mauaji  hayo bado   hakijajulikana  lakini  mke  wa mtuhumiwa alikuwa anatibiwa na John na mumewe alikuwa akimtuhumu   mganga huyo kuwa ana uhusiano wa kimapenzi na mke wake. Kamanda Mwaibambe alisema tukio la  pili lilitokea saa 8:30 usiku wa Januari 15 mwaka huu ambapo kundi la wahalifu wasiopungua 10 walimvamia  na kumuua   Onesmo Mutta ( 24 ) mkazi wa Mtaa wa Katotorwansi  kata ya Kashai Manispaa ya Bukoba. 
Alisema katika tukio hilo wahalifu  hao walivamia nyumba aliyokuwa akiishi  Mutta  ambayo ilikuwa na wapangaji  wengine na kuanza kuwapiga  na kudai kupatiwa fedha huku wakiwa wamebeba mapanga na marungu.
Alisema Mutta alichomwa na kitu chenye ncha kali kifuani upande wa kushoto  na kufa  papo hapo. Alisema  wapangaji wengine  watatu na mke wa Mutta walijeruhiwa sehemu  mbalimbali za miili yao. Wahalifu hao walifanikiwa  kuiba vitu mbalimbali  vyenye thamani  ya Sh 400,000.
Aliwataja waliojeruhiwa kuwa ni Philipina Onesmo mke wa Mutta ,Edwin Haipolite (23 ) mjasiriamali,  Adelene Simon (27 )n a Denice  Gervas.

No comments: