Watu
wanne wa familia moja wakazi wa kijiji cha Kibambila wilayani Kakonko mkoa wa
Kigoma wamekufa na mtu mmoja amenusurika kifo kutokana na kula chakula
kinachosadikiwa kuwa na sumu.
Akithibitisha kutokea
kwa tukio hilo, Mganga wa zamu katika Kituo cha Afya cha Kakonko, Ndalikunda
Kweka alisema kuwa watu hao walifikishwa kituoni hapo wakiwa na hali mbaya na
baadaye wote wanne walifariki dunia wakati wahudumu wa afya wakijitahidi kuokoa
maisha yao.
Mganga Mkuu wa wilaya ya
Kakonko, Fadhili Seleman aliwataja watu waliokufa kuwa ni Neema Joseph (12),
Jonas Joseph (18), Yusuph Joseph na Majaliwa Joseph (11).
Alisema kuwa uchunguzi
wa awali uliofanywa na wahudumu wa afya kituoni hapo na baada ya kumhoji mtu
aliyenusurika kwenye tukio hilo unaonesha kuwa watu hao walikula ugali
unaosadikiwa kuwa ulikuwa na sumu.
Baba mzazi wa watoto
waliokufa kwenye tukio hilo, Joseph Kajolo alisema kuwa aliweza kunusurika
kuingia kwenye janga hilo kwa kuwa siku ya tukio hakula chakula hicho kwa kuwa
alirejea nyumbani akiwa amelewa.
Mzazi huyo alisema kuwa
hata hivyo pamoja na kunusurika huko hajui kama sumu hiyo ilikuwa kwenye unga
uliotumika kupikia ugali huo au kuna mtu aliyeiweka baada ya ugali huo kupikwa.
Naye Mkuu wa wilaya ya
Kakonko, Peter Kiroya alisema kuwa polisi wilayani humo inamshikilia mtu mmoja
ambaye jina lake linahifadhiwa kwa sasa kutokana na sababu za kiusalama
akituhumiwa kuhusika kuweka sumu kwenye chakula hicho.
Sambamba na kukamatwa
kwa mtu huyo, Toyima ametoa wito kwa wakazi wa wilaya hiyo kuacha mchezo wa
kuwekeana sumu kwenye vyakula na kusababisha mauaji kwani kwa sasa tabia hiyo
imeanza kuota mizizi kwenye wilaya hiyo.
No comments:
Post a Comment