MAMA WA MAPACHA SITA AKABIDHIWA NYUMBA

Mkazi wa Mabwepande, Salome Muhando ambaye alitelekezwa na mumewe, baada ya kujifungua watoto sita mapacha mfululizo, hatimaye amenunuliwa na kukabidhiwa nyumba na Benki ya Covenant ambayo ataishi yeye na wanawe.

Alikabidhiwa nyumba hiyo katika eneo la Mabwepande wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam jana.
Alikabidhiwa nyumba hiyo na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki hiyo, Balozi, Salome Sijaona na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo, Sabetha Mwambenja.
Mwambenja alisema pamoja na kumkabidhi nyumba mama huyo, pia benki hiyo itampatia Bima ya Matibabu kutoka kampuni ya AAR, ambayo itamsaidia kupata huduma za matibabu yeye na watoto wake hao sita.
“Pamoja na kumpatia nyumba Salome,  pia tunampatia Bima ya Matibabu ambayo itamwezesha yeye na watoto wote kutibiwa katiba hopitali zote zilizo mahali popote nchini. Tuna uhakika sasa atakuwa na uhakika wa afya yake na watoto wake katika kipindi chote, hivyo atakuwa na nafasi ya kufanya shughuli zake za uzalishaji mali kwa amani,” alisema Mwambenja.
Kwa upande wake, Sijaona alisema baada ya kuona mateso ambayo mwanamke huyo alikuwa akiyapata kwa kukosa makazi, chakula na mahitaji mengine ya kibinadamu, benki hiyo iliona ni vyema kumsaidia, ikiwa ni sehemu moja ya kutimiza majukumu yake kwa jamii.
“Tumeguswa sana na mateso ambayo amekuwa akiyapata Salome Mhando pamoja na watoto wake baada ya kutelekezwa na mume wake kwa kigezo ha kuzaa watoto mapacha mfululizo, tuliguswa na kuamua kujitolea kumnunulia nyumba ambayo ataimiliki yeye mwenyewe,”  alisema Sijaona  ambaye ni Balozi wa Tanzania nchini Japan, Australia na New Zealand. 
Balozi Sijaona alisema “Nyumba hii tumemkabidhi pamoja na samani za ndani ambazo zitamwezesha sasa kuishi maisha ya amani na furaha akiwa kama wanawake wengine na kufurahi na watoto wake”.
Kwa upande wake,  Salome alidai alikimbiwa na mumewe, Ali Nassoro kutokana na kuzaa mapacha mfululizo; na kwamba baada ya kutelekezwa, alikuwa  akihifadhiwa kwa makazi na chakula na wanae na Mwinjilisti wa Kanisa la Waadventista Wasabato (SDA) la Mwenge, Sixberth Telugwa na mkewe.  Telugwa anafanya uinjilisti katika maeneo mapya ya Vikawe, Kimele, Bomafa na Mapwepande, anakoishi Salome.
Salome aliishukuru mno Benki ya Covenant kwa kumpa nyumba hiyo na kwamba sasa ana uhakika wa maisha yake na watoto wake.
“Naishukuru sana Benki ya Covenant kuniwezesha kumiliki nyumba yangu, ninawashukuru sana na ninaomba waendelee na moyo huo wa kuwasaidia kina mama wenye matatizo kama haya kwa sababu siko peke yangu,” alisema huku akiwa na mapacha wake, Martin na Helieth wenye miaka sita kila mmoja, Tatu na Nassoro wenye miaka minne na Eliya na Elisha wenye mwaka mmoja mmoja.

No comments: