Chama cha Wananchi -CUF kimeamua kuahirisha maandamano yake,
yaliyopangwa kufanyika jana, ikiwa ni ishara ya kuadhimisha miaka 14 ya vifo
vya wafuasi wake waliopoteza maisha Januari 27, mwaka 2001.
Hatua hiyo iliafikiwa na viongozi wa juu wa chama hicho baada ya
Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, kupiga marufuku maandamano hayo na
kubainisha kuwa ni batili.
Taarifa ya Jeshi la Polisi iliyotumwa katika ofisi za chama hicho,
ilitoa sababu tatu za kuahirisha maandamno hayo.
Sababu hizo ni maandamano hayo yaliyotarajiwa kufanyika jana
kuadhimisha mauaji hayo, yangeleta chuki ndani ya jamii, na pia sababu za
kiintelijensia zilionesha uwezekano wa kuwepo na vurugu na hali ya uvunjifu wa
amani, kutokana na matishio ya usalama na ugaidi, ambayo yanaweza kuhatarisha maisha ya waandamanaji.
Akitoa maazimio ya kuahirisha maandamano hayo, Mwenyekiti wa chama
hicho, Profesa Ibrahimu Lipumba alisema polisi hawajakitendea haki chama hicho,
kwani walichelewa kujibu maombi yao ya kufanya maandamano ya amani ya
kuadhimisha vifo vya ndugu zao na wafuasi wa chama chao.
“Polisi hawajakitendea haki chama chetu. Tokea siku ya Alhamisi
wiki iliyopita tulipeleka barua ya kuomba kibali lakini hadi jana saa kumi na
mbili ndio wanaleta taarifa ya kuahirisha maandamano na wakati huo viongozi
wote walishaondoka ofisini,” alisema Lipumba.
Alisema kuchelewa kwa taarifa hiyo, kulikuwa na nia mbaya na
wananchi, kwani wananchi walishajiandaa tayari kwa ajili ya kuandamana kwenye
maadhimisho hayo.
“Wananchi hawakuweza kupata taarifa ya kuahirishwa kwa maandamano
hayo na ndio maana leo wamefika hapa kwa wingi,” alisisitiza Lipumba.
Hata hivyo, mwenyekiti huyo alisema chama chake kina mipango mingi
ya maendeleo ya taifa, hivyo wameona ni vyema kuahirisha maandamano hayo ili
kutochafua taswira ya chama na kuwaomba wafuasi wake wawe watulivu na kuendelea
na shughuli zao za kawaida.
“Chama chetu kina malengo mazuri na taifa hili. Haitakuwa vyema
kuendelea na maandamano haya kwani yatasababisha kupigwa na kukamatwa na polisi
na hivyo kuvuruga kabisa mipango yetu ya maendeleo ya chama na taifa kwa
ujumla,” alisema.
Awali, kabla ya kuwasili kwa viongozi wakuu wa chama hicho,
wafuasi wake walionekana kuwa na jazba wakiwa wamebeba mabango yenye ujumbe
tofauti tofauti na huku wakiwa wamefunga vitambaa vyeusi kwenye mikono yao.
Maandamano hayo yalipangwa kuanzia ofisi za makao makuu ya chama
hicho Manispaa ya Temeke mtaa wa Boko na kumalizikia katika viwanja vya Zakhem
Mbagala.
No comments:
Post a Comment