JUKWAA LA KATIBA LATAKA WAGOMBEA KUPIMA AFYA

Jukwaa la Katiba nchini (JUKATA) limesema katika kuelekea Uchaguzi Mkuu wa taifa, ipo haja ya wagombea  wa nafasi mbalimbali za uongozi kupimwa afya zao na kutangazwa kwa wananchi ili kuepuka kuwaweka wagonjwa madarakani.

Mwenyekiti wa  Jukata, Deus Kibamba alisema hayo Dar es Salaam wakati akitoa tathmini ya uchaguzi wa marudio nchini Zambia kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, Michael Satta wa chama cha Patriotic Front  (PF).
Uchaguzi huo umefanyika kwa   mara ya pili ambapo  kabla ya Satta alitangulia Levy Mwanawasa  aliyefariki  akiwa katika nafasi ya urais Agosti mwaka 2008 na kusababsiha uchaguzi mdogo uliompa ushindi Rupiah Banda ambaye alishika nafasi hiyo kwa kipindi cha miaka miwili.
Kuhusu  kupima afya za viongozi nchini, alisema Jukwaa hilo linapendekeza Tanzania kuitazama Zambia kama mfano na kuanza kujihami kwa baadaye licha ya kwamba hakuna anayepanga jambo kama hilo kutokea.
“Tanzania kuna wagonjwa  wengi na wengine wanataka hata kuingia Ikulu …ni vyema afya zao zikapimwa na kutangazwa kwa wananchi ili kuepuka hatari ya kurudiarudia uchaguzi kama ambavyo imeikuta nchi ya Zambia,” alisema Kibamba.
Alisema  ni wakati sasa kwa wagombea wote kujitathmini na kujipima kabla ya kupitishwa, kufanyiwa uchunguzi  na kutambulika kuwa suala la afya za wagombea ni la kitaifa na si siri.
Kuhusu afya zitapimwaje alisema kwa Zambia  Tume ya Uchaguzi nchini humo iliteua Wakala wa Afya kwa ajili ya kupima afya za wagombea na kwa  hapa nchini ni vyema suala hilo likawa kama sharti ili kwa wale watakaoshindwa kutekeleza wakaachana na harakati hizo.
Alisema uchaguzi wa Zambia ulikuwa huru,  haki na wa kuigwa na nchi mbalimbali za Afrika kwa kuwa ulifanyika kwa uwazi huku Tume ya Uchaguzi ya nchini humo ikifanya kazi kwa umahiri na kutoa elimu kwa raia kwa kiwango kikubwa.
Akizungumzia kuhusu Kura ya Maoni ya Katiba Inayopendekezwa,  alisema hakuna haja ya kuharakishwa na kufanyika Aprili, mwaka huu kwa kuwa maandalizi ya kutosha hayapo huku pia nakala za Katiba hiyo zikiwa hazijafikishwa kwa wananchi na kuweza kuisoma na kuielewa.
Alisema hadi sasa maandalizi ya uboreshwaji wa daftari la wapiga kura halijafanikiwa, pia upo mchakato wa vitambulisho  vya Taifa unaoendelea na ambao haujaweza kusambaa mikoani tangu kuanza kwake ambapo ni vyema hatua ya Kura ya Maoni ikasimamishwa na kufanyika baada ya Uchaguzi Mkuu kumalizika.

No comments: