Waziri wa Elimu na Mafunzo
ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa amesema Serikali itazinyang'anya leseni ya
uendeshaji shule binafsi, ambazo zimeweka viwango vyake vya ufaulu kwa
wanafunzi wanaosoma kwenye shule hizo, tofauti na viwango vya Serikali.
Akijibu swali bungeni jana, Dk Kawambwa alisema iwapo shule hizo
zitashindwa kufanyia kazi maelekezo ya wizara yake, hakutakuwa na njia
nyingine, bali shule hizo kusitishiwa uendeshaji wake kwa kuzinyang'anya
leseni.
Dk Kawambwa alitumia fursa
hiyo, kuonya shule binafsi kuhakikisha zinatekeleza maagizo ya Serikali ambayo
yanazitaka kusitisha mfumo wake wa kuweka viwango vyao vya alama ya ufaulu wa
mitihani.
Waziri huyo alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Conchesta Rwamlaza (Chadema) ambaye alikuwa
anataka kufahamu kama Serikali inafahamu kwamba shule binafsi zimeweka viwango vyao wa alama za ufaulu.
Katika swali lake, Rwamlaza aliongeza kuwa wanafunzi ambao wanashindwa
kupata alama zilizowekwa na shule binafsi, wanalazimishwa kukariri darasa au
kufukuzwa shule.
Alisema hali hiyo imekuwa inawaathiri wazazi ambao wanapata mzigo
wa kuendelea kulipa ada, lakini pia hali hiyo inawapotezea muda wanafunzi hao.
“Hizi shule binafsi kwanza
ada zake ziko juu; lakini pia zina mfumo wao nje ya mfumo wa Serikali ambao
unawaathiri wanafunzi na wazazi. Wengi wa wanafunzi ambao wanashindwa kufikisha
alama zilizowekwa na shule husika wanalazimishwa
kurudia darasa," alisema.
Aliongeza kuwa imefikia kiwango hata wanafunzi ambao wako kidato
cha nne, ambao wanategemea kufanya mtihani wa kitaifa wanafukuzwa kwa sababu tu
wameshindwa kufikisha ufaulu wa alama zilizowekwa na shule binafsi.
Kwa hali hiyo mbunge huyo, alitaka kufahamu hatua zinazochukuliwa
na Serikali kuhakikisha mfumo huo unapigwa marufuku na Serikali.
Katika majibu yake, Dk Kawambwa aliwaelekeza maofisa elimu wa
mikoa na wale wa wilaya, kuhakikisha shule zote za Serikali za binafsi
zinatekeleza maagizo ya Serikali ambayo yametolewa na wizara hiyo inayosimamia
utoaji wa elimu na sio vinginevyo.
“Kuna maelekezo mengi
ambayo tumeyatoa kwa shule zote likiwemo hili la alama za ufaulu na shule
binafsi zinatambua hilo kwamba zikienda kinyume na agizo la wizara hatua
inayofuata ni kufungwa kwa shule hizo," alisema Dk Kawambwa.
Alisema hakuna njia nyingine kwani serikali inataka kuhakikisha
kwamba maelekezo yake yanatekelezwa.
Alitoa mwito kwa wananchi kutoa taarifa kwa shule ambayo inafanya
mambo kinyume na maagizo hayo ya serikali ili hatua ziweze kuchukuliwa.
No comments:
Post a Comment