Kijana ambaye hakufahamika jina anayekadiriwa kuwa na umri kati ya
miaka 30 hadi 35 amekutwa ameuawa na mwili wake kutelekezwa katika eneo la
kambi ya Polisi Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) kata ya Nshambya mkoani
Kagera.
Mwili huo uligundulika majira ya saa sita mchana baada ya watu
waliopita katika eneo hilo kuuona ukiwa umelazwa karibu na moja ya shamba
lililopo mtaa wa Bunkango eneo la kambi hiyo ya Polisi.
Mwandishi alishuhudia mwili huo ulioanza kuharibika ukiwa
umevuliwa nguo zote ukiwa bado haujaondolewa katika eneo hilo la tukio.
Mwili huo ulikuwa na majeraha maeneo ya usoni kiasi cha kushindwa kutambulika kirahisi.
Akizungumza na waandishi wa habari waliofika katika eneo hilo,
Kaimu Mtendaji wa kata ya Nshambya, Christian Ngaiza, alisema alipata taarifa
za tukio hilo kutoka kwa dereva wa bodaboda kuwa kuna mtu ameuawa lakini
wananchi wanaogopa kutoa taarifa
Polisi.
Ngaiza, alisema baada ya
kupata taarifa hiyo aliamua kwenda eneo
la tukio majira ya saa saba mchana na kutoa taarifa ya tukio hilo Polisi.
Aidha, alisema baada ya kubaini mwili huo, alianza uchunguzi na
kuhoji wananchi wa mitaa yote mitatu ya eneo hilo endapo wana taarifa za mtu
yeyote aliyepotea ambapo ilibainika hakukuwa na mtu aliyepotea.
Mkazi wa Mtaa wa Migera, Joyce Nuru, akizungumzia tukio hilo,
alisema alipata taarifa za kukutwa kwa maiti huyo, akiwa nyumbani kwake ambapo
majira ya saa sita mchana wanafunzi
walipita na kumueleza kuwa kuna mtu amekufa maeneo ya
mnara.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera ambaye pia ni mpelelezi wa
makosa ya jinai mkoani humo, Gilles Mroto
alisema tukio hilo amelisikia na ametuma timu ya maofisa wa Polisi
kwenda eneo la tukio kufanya uchunguzi.
Hata hivyo, mwili huo haukuweza kutambulika na hivyo kuzikwa na
Manispaa ya Bukoba katika makaburi ya Kyebitembe.
No comments:
Post a Comment