Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma
litawaweka kiti moto watuhumiwa 9 ambao
ni viongozi wanaohusishwa na kashfa ya akaunti ya uchotaji wa fedha kutoka
kwenye akaunti ya Tegeta Escrow.
Viongozi hao watawekwa kiti moja kwa uwazi
mwanzoni mwa mwezi ujao kwenye ukumbi wa Karimjee, Dar es Salaam. Habari
zinaeleza kuwa watakaoitwa ni wale viongozi wote ambao wanaowajibika chini ya
Sheria ya maadili ya viongozi wa umma.
Taarifa zilizopatikana kutoka ndani ya tume ya
maadili zilieleza kuwa kwa sasa hati za kuitwa kwa watuhumiwa hao zinaandaliwa,
lakini hata hivyo tume hiyo haikutoa majina ya watuhumiwa hao.
Hata hivyo sheria ya maadili ya viongozi wa
umma inawabana viongozi na watumishi wa ngazi ya juu wa umma wakiwemo wabunge,
majaji, wakuu wa wilaya, mikoa, majaji na mawaziri, mwanasheria mkuu.
Licha ya majina ya watuhumiwa hao
kutopatikana, lakini chini ya sheria hiyo viongozi wanaowajibika kwa tume hiyo
wako 27 na miongoni mwao wamo wabunge, wakuu wa wilaya, majaji na hakimu na
katibu mkuu wa wizara.
Kwa hali hiyo wabunge ambao wanatarajia
kusimama mbele ya tume hiyo ni wale ambao walipokea fedha kutoka kwa mmiliki wa
kampuni ya VIP Engineering James Rugemarila ili waeleze mazingira ya kupewa
fedha hizo.
Wabunge hao ni Mbunge wa Bariadi Magharibi
Andrew Chenge aliyepokea Sh bilioni 1.6,
Mbunge wa Sengerema William Ngeleja ( Sh milioni 40), Mbunge wa Muleba Kusini
Profesa Anna Tibaijuka ambaye alipokea Sh bilioni 1.6 na akajitetea kuwa fedha
hizo zilikuwa ni za mchango wa kulipa mkopo wa shule anayoisimamia.
Pia Profesa Sospeter Muhongo ambaye amejiuzulu
uwaziri wa nishati na madini hivi karibuni; lakini anabakia na ubunge wake pia
anaweza kuitwa mbele ya tume hiyo aeleze mazingira ya kuruhusu fedha
zilizokuwemo kwenye akaunti ya Tegeta Escrow zichotwe kirahisi.
Wengine ni majaji Frederick Werema ambaye
alikuwa mwanasheria mkuu wa Serikali naye ataeleza sababu za kuamuru fedha hizo
za Escrow zichotwe. anabanwwa na kipengele kinachoeleza kuwa anatakiwa kutoa
maamuzi kwa mujibu wa sheria za nchi.
Jaji Werema katika sakata hilo anatuhumiwa
kuvunja sheria za nchi kwa kuruhusu fedha hizo zichotwe bila kutozwa kodi jambo
ambalo Mamlaka ya Mapato imedai kulikuwa na kodi ya Serikali.
Majaji wengine ni Dk John Ruhangisa na
Aloycsius Mujulizi. Dk Ruhangisa na Mujulizi wao wamekiri kupokea fedha kutoka
kwa Rugemarila. Dk Ruhangisa alipokea Sh Sh404.25 milioni na Jaji Aloysius K
Mujulizi (Sh40.4 milioni).
Pia yumoa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usajili wa
Vizazi na Vifo (Rita), Philip Saliboko (Sh40.4 milioni) ambaye anabanwa na
sheria hiyo pia anaweza kuitwa na tume hiyo.
Wabunge na majajji ambao wamekiri kupokea fedha hizo
wanabanwa na kipengele kinachoeleza zawadi na fadhila kw aviongozi wa umma kuwa
wanatakiwa wasiombe wala kupokea fadhila za kiuchumi zaidi ya zawadi ndogo
ndogo ukarimu wa kawaida au fadhila nyingine za zawadi za kawaida.
Pia Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini
Eliakim Maswi naye anaweza kuitwa kwenye tume hiyo kwa kuwa bado ni mtumishi wa
serikali ambaye anaendelea kuchunguzwa. Naye anabanwa na kipengele cha utoaji
wa maamuzi aliyoyafanya akiwa madarakani.
Kamishna wa Tume ya Maadili Jaji Mstaafu
Salome Kaganda licha ya kukiri kuwepo kwa suala hilo lakini hakutaka kutoa
ufafanuzi wa kina, lakini taarifa kutoka ndani ya ofisi ya tume ya maadili zinasisitiza kuwa kikao hicho
kitafanyika mwanzoni mwa mwezi ujao .
Katika kikao hicho pia
viongozi wengine wawili ambao ni Mkuu wa Wilaya ya Korogwe Mrisho Gambo ambaye
ataendelea kubanwa na tume hiyo kwa
madai ya matumizi mabaya ya madaraka pamoja na Meya wa Manispaa ya Tabora
Gullam Hussein Dewji ataendelea kubanwa juu ya ufujaji wa fedha za manispaa
anaodaiwa kuufanya.
No comments:
Post a Comment