KARIAKOO WAFUNGA MADUKA, WAANDAMANA KUMSAKA BOSI WAO


Wafanyabiashara wa Soko la Kariakoo jijini Dar es Salaam, wameandamana hadi kituo cha Polisi cha Kati, wakidai wapewe taarifa wapi alipopelekwa Mwenyekiti Taifa wa Jumuiya ya Wafanyabiashara,  Johnson Minja.

Baadhi ya wafanyabiashara hao  walifunga maduka yao na kuandamana wakishinikiza kuachiwa huru kwa Minja, ambaye aliondolewa katika Kituo cha Polisi Kamata bila taarifa rasmi.
Maandamano hayo ya wafanyabiashara, yalikumbana na ulinzi mkali wa askari nje ya jengo la Kituo cha Kati na kuishia nje.
Hata hivyo, baadaye baadhi ya viongozi wao walifanikiwa kuingia na kufanya mazungumzo na Naibu Kamishna Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Simon Siro ambaye aliwaeleza kuwa Minja amepelekwa Dodoma, ambako ndiko iliko kesi iliyomfanya akamatwe.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya wafanyabiashara kujaa maeneo ya kituo hicho cha Polisi, Kamanda Siro alithibitisha kupata taarifa ya maandamano hayo na pia kushikiliwa Minja na Jeshi hilo ambapo alisema amepelekwa Dodoma na kwamba yuko salama.
“Ni kweli Minja amekamatwa lakini tukio lililomfanya akamatwe alilifanya Dodoma, amesafirishwa kupelekwa huko ambako kesi yake iko na kesho atafikishwa mahakamani,” alisema Kamanda Siro.
Siro alilaani kitendo cha wafanyabiashara hao kufunga maduka na kufanya maandamano ambayo ni kinyumwe cha sheria.
“Wangenipigia simu tu na kuniuliza, lakini sio kufunga maduka na kufanya maandamano, kitu walichofanya sio kizuri na kwasababu ni mara ya kwanza tumewasamehe, Minja yupo salama ila amepelekwa Dodoma kwenye kesi yake ya uchochezi,” alisema Siro bila kufafanua zaidi ni uchochezi wa aina gani.
Akizungumza na mwandishi, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya wafanyabiashara Tanzania, Mchungaji Silver Kiondo alisema wamepewa maelezo ya kwamba Minja amepelekwa Dodoma hivyo wameamua kuondoka eneo hilo la kituo cha Polisi Kati ili wajipange  kusafiri kwenda Dodoma kumtolea dhamana.
“Baada ya kupata taarifa kutoka kwa Kamanda Siro kwamba Minja yuko Dodoma, tumewatangazia wafanyabiashara walioko hapa na tumeamua kuondoka,” alisema Kiondo huku wakiondoka wakiwa wameandamana, lakini bila kelele yoyote wakielekea Kariakoo.
Kiondo alisema jambo ambalo liliwashtua wafanyabiashara ni Minja alikamatwa juzi na Polisi na alitakiwa kuchukuliwa maelezo akiwa na mwanasheria wake. Lakini, asubuhi baadhi ya viongozi walifika wakiwa na mwanasheria kituo cha Polisi Kamata alikokuwa, lakini hawakumkuta, wakaambiwa amepelekwa Dodoma bila maelezo yoyote zaidi.
Waliporudisha taarifa hizo kwa wafanyabiashara, waliamua kuja kituo cha Kati kupata taarifa zenye uhakika, kama kweli amepelekwa Dodoma ambapo wamethibitishiwa hilo na kuelezwa kwamba kesi yake inadhaminika wanaweza kwenda kumdhamini.
“Wafanyabiashara walipata wasiwasi hivyo tukaamua kuja kupata taarifa hapa, wametuthibitishia kwamba yuko salama, tunaweza kwenda Dodoma kumuwekea dhamana na mambo mengine yaendelee,” alisema Kiondo.
Alisema kuridhika kwao ni mpaka watakapomuona Minja akiwa salama, ndio maana wameamua kwenda Dodoma baada tu ya kutoka hapo Polisi na kuhakikishiwa yuko Dodoma.
 “Hatuwezi kusema tumeridhishwa na kauli za polisi, kuridhika kwetu ni kumuona Minja tunafanya utaratibu hapa wa kwenda Dodoma,” alisema.
Alisema hofu waliyonayo ni watu kadhaa wamekuwa wakikamatwa na wanakuwa katika hali za utatanishi, hivyo na wao wana kila sababu ya kuwa na hofu na kiongozi wao mpaka pale watakapomuona akiwa salama.

No comments: