Ofisi ya Waziri
Mkuu,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) imepeleka suala la
mchakato wa uuzaji wa hisa za Halmashauri ya jiji la Dar es Salaam katika
Shirika la Usafiri Dar es Salaam(UDA) kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na
Rushwa (Takukuru) ili kuangalia mchakato mzima na mkanganyiko katika uuzwaji wa
hisa hizo.
Pia wamemtaka
mwanasheria mkuu wa serikali kuupitia mchakato
mzima kubaini kama hisa hizo zimeuzwa kwa kampuni ya Simon Group au hazijauzwa.
Akijibu hoja za
kamati ya Bunge ya Kudumu ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) kuhusu mikataba
yenye maslahi duni kwa halmashauri, Waziri wa Tamisemi, Hawa Ghasia (pichani) alisema
kupelekwa kwa suala hilo Takukuru pamoja na kwa mwanasheria mkuu wa serikali,
ni kutaka kubaini kama hisa hizo ziliuzwa au la na kama ziliuzwa ilikuwa
kihalali?
“Suala hili la
UDA tumeamua kulipeleka kwa Mwanasheria Mkuu wa serikali na Takukuru kujua
uhalali wa mchakato mzima wa uwekezaji na iwapo mauzo ya hisa za jiji yaliuzwa
kihalali au la?,” alisema.
Awali,
Mwenyekiti wa kamati hiyo ya LAAC, Rajab Mbaruk
Mohamed akiwasilisha taarifa yake ya hesabu za serikali za mitaa kwa
mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, mwaka 2013. Alitaka serikali kueleza ukweli
kama hisa za jiji katika UDA zimeuzwa na kuhamishiwa kwa mwekezaji huyo au
hazijauzwa.
Kamati hiyo
ilisema endapo hisa hizo hazijauzwa, mchakato wa uuzaji wa hisa hizo utapaswa
kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zinazohusika.
Lakini wakati
mijadala inaanza, Mbunge wa Ilala, Mussa Azzan
Zungu alipotaka kujadili suala hilo la UDA, Spika wa Bunge Anne Makinda
alimzuia na kueleza kuwa hairuhusiwi
kulijadili kutokana na kuwa serikali walimpelekea taarifa ya kuwepo kwa
kesi mbili zinazohusu UDA, hivyo kujadili watakuwa wameingilia uhuru wa
Mahakama.
Uamuzi huo
uliungwa mkono na Mwanasheria Mkuu wa serikali, George Masaju aliyesema hata
yeye anayo mashauri matatu ya UDA mahakamani hivyo kwa utaratibu wa kuheshimu
mihimili mwingine ni vema suala la UDA lisijadiliwe.
Akizungumzia
suala la Halmashauri ya Kinondoni kutonufaika na uwekezaji wa kampuni ya
Oysterbay Villas, alisema ukwamishaji wa Kinondoni ulitokana na mkataba
waliokubaliana lakini baada ya wiki moja Halmashauri ya Kinondoni itaanza
kunufaika na uwekezaji huo ulioanza mwaka 2010.
Ghasia alisema
ili kuondokana na mikataba yenye utata katika Halmashauri, imeamuliwa mikataba
yote kupitia kwa Mwanasheria Mkuu wa serikali kujua kama mikataba hiyo ina
manufaa hivyo malalamiko hayo hayatarudia.
No comments:
Post a Comment