MIJADALA YA WIZI, UFISADI SASA YAWACHOSHA WABUNGE


Wabunge wameelezea kuchoshwa na wizi, matumizi mabaya ya fedha na mikataba mibovu iliyobainishwa katika taarifa za baadhi ya kamati zilizowasilishwa bungeni, na kushauri maazimio yapitishwe ili wahusika wa ufisadi huo wabanwe.

Katika kuchangia taarifa za Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) pamoja na Kamati ya Bajeti zilizowasilishwa bungeni,  wabunge wengi wameeleza kuchoshwa na mijadala ya kila mara bungeni inayohusu  wizi na ufisadi, badala ya kujadili maendeleo ya wananchi.
Kwa mujibu  wa wabunge hao, katika taarifa zote zilizowasilishwa, suala la wizi  na matumizi mabaya ya fedha za Serikali limejitokeza kwa wingi, jambo ambalo wabunge wametaka hatua za makusudi zichukuliwe haraka, kuliko wabunge kuendelea kulalamika bila kupata suluhu la kudumu.
Mbunge wa Mkanyageni, Habib Mnyaa (CUF) alitoa mfano wa suala Kampuni ya Ndege (ATCL) lililoainishwa kwenye taarifa ya PAC juu ya  hali ya kifedha na madeni makubwa iliyo nayo.
Madeni hayo ni pamoja mabilioni ya fedha yanayoendelea kulipwa kwa Kampuni ya Wallis, kwa huduma ya ndege iliyofanya kazi nchini kwa miezi sita pekee, na kisha ndege kupelekwa Ufaransa kwa matengenezo.
Alisema chanzo cha tatizo ni mikataba mibovu. “Tulidai mikataba iletwe bungeni tuipitie. Ikiwa tutaendelea kulalama kwamba tunaibiwa… wizi kila mahali, ikiwa hatutasaidia Takukuru (Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa) kama Bunge kwa kuona kwamba wote waliohusika na mikataba wanafikishwa mahakamani, itakuwa Bunge hatujatenda haki.
“Kwa kamati ambazo zimewasilisha taarifa, tupitishe maazimio kwa mikataba yote yenye utata na walioipitisha, wafikishwe mahakamani. Tulione Bunge likiwa na meno yake, wote waliohusika wachukuliwe hatua kwa kupelekwa mahakamani,“ alisema.
Mbunge wa Viti Maalumu, Ester Bulaya (CCM), alizungumzia suala la Mamlaka ya Bandari (TPA) kutumia Sh bilioni tisa kulipana posho bila kuidhinishwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina; taarifa iliyotolewa na PAC.
Bulaya alihoji majibu ya Waziri wa Fedha, Saada Mkuya, ambaye juzi katika kujibu, alisema TPA walijieleza kwamba walifanya hivyo kutokana na kutokuwa na uelewa wa sheria. “Eti jibu jepesi,  hawakuwa na uelewa wa kisheria!. Tunaomba watu wote hao washughulikiwe. Haiwezekani makosa yawe yale yale na majibu yale yale,” alisema Bulaya.
Kuhusu madeni ambayo mifuko ya hifadhi ya jamii inadai Serikali, Bulaya alisema; “Kila siku zinapigwa kelele juu ya hali mbaya ya mifuko ya jamii, halafu Waziri anasema kinaundwa kikosi kazi…hiki ni kikosi kazi cha kumi, hivyo tisa havijajua tunadaiwa kiasi gani?”
Kwa upande wa jengo la watu mashuhuri katika Uwanja wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, mbunge huyo alihoji  uhalali wa kutumika Sh  bilioni 12 kwa ujenzi wake.
“Dili  nyingine ukipewa funga mikono, nawa mikono zinagusa maisha ya watu maskini,” alisema.
Bulaya ambaye pia alihoji sababu za asilimia 10 ya fedha za akina mama na vijana kutotengwa kwenye halmashauri, alishauri mawaziri kubana watendaji  iwapo hawataki kupigiwa kelele bungeni.
Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema), alisema iwapo wizi hautadhibitiwa, nchi haiwezi kubadilika hata ikikusanya matrilioni ya shilingi.
“Ni lini tutajadiliana bungeni bila kujadili wizi? Ifike hatua tujadili sera za kuendeleza Taifa,” alisema Mbunge huyo na kuongeza kuwa CUF na Chadema haviko kwa ajili ya kushika madaraka tu, bali ni kwa ajili ya kuwezesha taifa kwenda mbele. Aliongeza kuwa kama CCM ikiongoza vyema kukawa na maendeleo, itakuwa sawa.
Alisema katika taarifa ya PAC mwanzo hadi mwisho, kinachosomwa zaidi ni wizi, jambo alilotaka Serikali kushughulikia watu wanaojenga nyumba kwa mikataba ya uongo sanjari na ulipaji mishahara hewa.
Pia Mbunge wa Nkenge, Asumpta Mshama (CCM) alihoji ni lini bunge litaelezwa kwamba matumizi ya fedha sasa yanakwenda vizuri.
Mshama alishauri sheria ya ununuzi iletwe bungeni waibadilishe kwa kile alichosema, inatoa mwanya mkubwa wa kufanya matumizi mabaya ya fedha.

No comments: