WATENDAJI WA HAZINA WAFUTIWA UKURUGENZI MASHIRIKA YA UMMA


Serikali imezuia watendaji wote wa Msajili wa Hazina, kuingia katika bodi yoyote ya mashirika ya umma kuepuka mgongano wa maslahi.

Waziri wa Fedha, Saada Mkuya (pichani) alisema bungeni, kwamba wameshaanza kuondoa watendaji hao katika bodi mbalimbali, ili kuhakikisha wafanyakazi wa Msajili wa Hazina, ambaye ndiye mwenye hisa katika mashirika yote ya umma, wanakuwa wasimamizi badala ya sehemu ya mashirika wanayoyasimamia.
Alikuwa akizungumzia taarifa ya Kamati ya Fedha za Serikali (PAC), iliyoonesha upungufu uliojitokeza katika ukaguzi maalumu wa matumizi ya Serikali na mashirika ya umma, ikiwemo Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA).
Katika ukaguzi huo, ilibainika kuwa Mamlaka hiyo ilitumia Sh bilioni 9.6 kwa ajili ya vikao vya wafanyakazi na mamilioni mengine yalilipwa kwa ajili ya posho za safari bila kibali cha Serikali.
Waziri Mkuya alikubaliana na taarifa ya PAC, kwamba Mamlaka hiyo iliidhinisha na kuanza kulipa malipo na viwango vipya vya posho ya safari ya kujikimu kwa watumishi, bila ya kupata kibali cha Msajili wa Hazina.
“Kwa mujibu wa Sheria ya Msajili wa Hazina, mashirika yana wajibu wa kupata kibali cha Hazina kabla ya kulipa mishahara na posho,” alisema Mkuya.
“Sisi Wizara ya Fedha, tumeshaamua rasmi kwamba watendaji wote wa Msajili wa Hazina hawatakuwamo katika bodi zozote za shirika lolote hapa Tanzania,” alisema Waziri Mkuya.
Alisema wamefanya hivyo kwa sababu kuruhusu wawemo kwenye bodi za mashirika, kutasababisha mgongano wa maslahi, kwani mfanyakazi wa Hazina anatakiwa kusimamia mashirika hayo.
Alifafanua kuwa kama hali hiyo ya mfanyakazi wa Hazina kuwa mjumbe wa bodi za mashirika ya umma itaachwa, badala ya mfanyakazi huyo kuwa msimamizi wa mashirika hayo, atakuwa sehemu ya matatizo yanayotokea kwenye mashirika.
“Tunaanza kuwatoa rasmi wafanyakazi wote katika bodi za mashirika. Tunaanza sasa hivi,” alisisitiza.
Hatua iliyochukuliwa na Waziri Mkuya, imelishinda Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambalo tangu mwaka Aprili 2010, aliyekuwa Mkaguzi  na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh, alitaka wabunge waondolewe mara moja katika bodi za wakurugenzi kwa kuwa kuwapo kwao katika bodi hizo, kunasababisha mgongano wa kimaslahi.
“Mwenendo huu ni kinyume na taratibu nzuri na ni kinyume na kanuni za utawala bora… wenzetu wanatucheka katika hili,” alisema Utouh alipokuwa akizungumzia ripoti yake iliyoishia Juni 30, 2009 ya ukaguzi wa mashirika ya umma na taasisi nyinginezo za Serikali.
Alisema wakati umefika kwa Serikali kutoa waraka ambao utazuia wabunge kuwa wajumbe wa bodi za wakurugenzi za mashirika ya umma, ili wahoji vyema mwenendo wa mashirika hayo.
Kutokana na hali halisi ya kutokuwepo maadili ya kutosha ya viongozi, hata Serikali imeliona na tangu mwaka jana ilishaanza kufanyia kazi mapendekezo ya kuundwa kwa Sheria Mpya ya Mgongano wa Maslahi Miongoni mwa Viongozi na Watumishi wa Umma.
Katika mapendekezo hayo yanayofanyiwa kazi chini ya Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Sheria hiyo imetakiwa itoe tafsiri ya dhana ya Mgongano wa Maslahi.
Bango kitita la mapendekezo hayo, limebainisha kuwa mpaka sasa hakuna Sheria inayotoa tafsiri ya dhana ya Mgongano wa Maslahi, hivyo kusababisha baadhi ya viongozi na watumishi wa umma kuingia katika tatizo hilo, kwa kukosa uelewa au kutumia mwanya wa ukosefu wa tafsiri hiyo kujinufaisha.
“Kukosekana kwa tafsiri  ya Mgongano wa Maslahi ni miongoni mwa sababu  zinazosababisha  baadhi ya  viongozi au watumishi wa umma  kutafsiri neno hilo kwa jinsi wanavyoona inafaa na hivyo kujinufaisha binafsi,” bango kitita hilo limeeleza.
Tafsiri inayopendekezwa ya dhana hiyo ya Mgongano wa Maslahi katika bango kitita hilo, imetajwa kuwa ni hali inayojitokeza wakati kiongozi au mtumishi wa umma, ambaye anayo maslahi katika jambo fulani, anapotekeleza majukumu yake au kufanya uamuzi, na katika kufanya hivyo anatumia nafasi hiyo kuendeleza maslahi yake binafsi au ya ndugu zake au marafiki zake kinyume cha taratibu za kazi yake. 

No comments: