POLISI YASEMA MADAI YA UTEKAJI MABASI ARUSHA YAMEJAA UTATA

Polisi Mkoa wa Arusha limeahidi kufanya doria katika barabara ya Arusha – Namanga ikiwa ni njia mojawapo ya kudhibiti vitendo vya kihalifu vinavyofanywa na watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi.

Juzi, watu hao waliteka magari na kupora abiria, huku likikiri tukio la kutekwa mabasi usiku huo limejaa utata. 
Uamuzi huo wa polisi mkoani Arusha ni kufuatia mabasi ya abiria kutoka Nairobi, Kenya kutekwa na kundi la watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi kuwapora abiria kiasi kikubwa cha fedha. 
Akizungumzia tukio hilo jana jijini hapa, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Liberatus Sabas alisema; “Kwa kifupi kuwa tukio hilo limejaa utata na linafanyiwa uchunguzi wa kina kabla ya taarifa rasmi kutolewa kwa umma. 
Alisema magari mawili kati ya yale yaliyotekwa yalikuwa na wafanyakazi na mizigo peke yake. 
“Acheni tumalize uchunguzi, tutawaambia kila kitu ,ila tumeongeza nguvu ya ulinzi katika njia hiyo,” alisema Kamanda Sabas na kuyataja mabasi yaliyotekwa kuwa yanamilikiwa na kampuni za Perfect, Dolphin,  Taqwa na Spider  ambazo mabasi yake yanafanya safari zake kati ya Arusha na Nairobi, Kenya. 
Tukio hilo lilitokea  juzi usiku  baada ya watu wanaokadiriwa kuwa zaidi ya 50 kuteka mabasi ya abiria katika eneo la Mbuga Nyeupe katika barabara ya Arusha- Namanga  na kupora kiasi cha fedha ambacho mpaka sasa hakijaweza kufahamika. 
Watekaji hao wanaodaiwa kuwa na silaha za moto na za jadi zikiwemo mapanga, visu na mashoka walifunga barabara kwa mawe ili kufanikisha utekaji wao.

No comments: