BALAA!! MISAMAHA YA KODI YAPAA KWA SHILINGI BILIONI 340

Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) imeitaka Serikali kufanya kila linalowezekana inapunguza misamaha ya kodi ambayo katika mwaka wa fedha 2013/14  ilipaa kwa Sh bilioni 340 kutoka Sh trilioni 1.48 hadi Sh trilioni 1.82 mwaka uliopita.
Mwenyekiti wa PAC Zitto Kabwe, alionesha wasiwasi kuwa kitendo cha kuchelewesha kutumika kwa  Sheria mpya ya Kodi la Ongezeko la Thamani (VAT) ya mwaka 2014, inachangia kuifanya Serikali izidi kupoteza mapato mengi kupitia kodi ya VAT katika mwaka huu wa fedha.
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato (TRA), Rished Bade aliiambia kamati hiyo kuwa misamaha ya VAT ilifikia Sh bilioni 676 katika mwaka wa 2013/14 kutoka Sh bilioni 571 ya mwaka 2012/13.
“Ni kweli misamaha ya kodi kila mwaka inaongezeka licha ya PAC kutaka tuipunguze, ongezeko hili linatokana na kuwepo kwa miradi mikubwa ambayo wahisani wanaifadhili na hivyo kuwa na sifa ya kupata msamaha wa kodi.
“Uchimbaji wa gesi na mafuta pamoja na ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi asilia kutoka Mtwara kuja Dar es Salaam pamoja na ujenzi wa daraja la Kigamboni ni miongoni mwa miradi mikubwa  ambayo ilifaidika na misamaha ya kodi," alisema Bade.
Ufafanuzi huo wa kamishna ulitokana na swali kutoka kwa Mbunge wa Viti Maalumu,  Esther Matiko (Chadema) ambaye alitaka kujua kwa nini kuna ongezeko la misamaha ya kodi kila mwaka hali ambayo inaifanya nchi kupoteza mabilioni ya fedha.
Kuanzia mwaka 2012, Kamati ya PAC ilimwelekeza Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya ukaguzi maalum juu ya misamaha ya kodi kama baadhi yake ina manufaa kwa nchi.
Ofisa kutoka ofisi ya CAG aliiambia kamati ya PAC kuwa ukaguzi huo utakamilika hivi karibuni na ripoti yake itakabidhiwa kwa kamati hiyo mwaka huu. “Kwa sasa tunafanya mapitio ya ubora wa ripoti hiyo ya ukaguzi  na itakuwa tayari Januari 22."
Kwa mujibu wa Bade, misamaha ambayo zilipata kampuni kubwa ambazo zinaendesha utafutaji na uchimbaji wa mafuta ambao unafanywa kwenye kina kirefu cha bahari inafikia Sh bilioni 100 wakati mashirika ya ndani ambayo yanaendesha miradi mbalimbali yalipata msamaha wa kodi wa Sh bilioni 147.
“Habari njema ni kwamba sheria mpya ya VAT ambayo itaanza kutumika hivi karibuni  itaondoa baadhi ya misamaha na hii itasaidia kupunguza misamaha hii," alisema Kamishna Mkuu wa TRA.
Wakati huohuo, Zito alisema Kamati yake itamwandikia Spika wa Bunge juu ya fedha zaidi ya Sh trilioni 1.7 ambazo ni mapato ya serikali ambayo yamekwama kutokana na kuwepo kwa kesi mahakamani.
 “Hizi ni pesa nyingi, tutamwandikia Spika ili aweze kutuandalia kikao na Waziri Mkuu na Jaji Mkuu kuangalia namna ambavyo suala hili linaweza kutatuliwa," alisema. “Ni vyema kesi hizi zikamalizika, tukishinda tutapata  kodi yetu na kama tukishindwa sawa lakini cha msingi ni hizi kesi zimalizike kusikilizwa," alisema.
Wakati Kamati ya Zitto ikilia na misamaha ya kodi, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (LAAC), Rajab Mbarouk Mohammed, amesema ni vyema watendaji wa Serikali wasiowajibika ipasavyo wakachukuliwa hatua za kisheria kwa udanganyifu na wizi badala ya kuwaonea ‘Panya Road’. 
Aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati kamati hiyo ilipokuwa inapitia hesabu za Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda ambapo ilibainika kuwa halmashauri hiyo haijawasilisha kwa mujibu wa Sheria kiasi kikubwa cha fedha za vijana na wanawake. 

“Naungana asilimia 100 na masuala ya ‘Panya Road’, kwa hali hii ninayoiona kwa watendaji wetu. Ingawa sikubaliani na wanayoyafanya kama vile kupora na kudhuru watu,” alisema. 

Alisema inasikitisha kuona baadhi ya watendaji wasiowajibika na kutimiza wajibu wao wakati Serikali imekuwa ikijitahidi na kuweka taratibu nzuri kuwezesha wananchi wake. 

“Ndio maana nasema ni jukumu la mamlaka husika kuchukua hatua  kwa watendaji kama hawa si kuwaonea hawa Panya Road,” alisema. 

Kwa mujibu wa hesabu hizo, halmashauri hiyo ilitakiwa katika mwaka wa fedha 2012/13 kuwasilisha kwa vijana Sh milioni 101 na badala yake imewasilisha kwa vijana hao Sh milioni saba tu huku ikikiri kuzitumia fedha hizo katika maeneo mengine. 

 “Kamati hii inaagiza mkatengeneze hesabu na taarifa zenu vizuri mkiwa na michanganuo ya madeni yenu yote na namna mtakavyoyalipa,” alisisitiza. 

Hatahivyo, Kamati hiyo iliipongeza halmashauri hiyo kwa kupokea hati safi ya hesabu zake kwa miaka mitatu mfululizo. 

No comments: