MKAZI WA DAR APANDISHWA KIZIMBANI KWA TUHUMA ZA UGAIDI

Mkazi wa Kitunda, Jihad Swalehe amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na mashitaka ya Ugaidi na kuomba msaada  wa vifaa, fedha na ujuzi wa kulipua mabomu kwa lengo la kuwadhuru  watu wa Kenya.
Swalehe alifikishwa mahakamani hapo na kusomewa mashitaka na Wakili wa Serikali Peter Njike mbele ya Hakimu Mkazi Emilius Mchauru.
Wakili Njike alidai, kati ya Machi 21 mwaka juzi na Juni 2 mwaka jana katika maeneo tofauti tofauti Dar es Salaam, Swalehe na wenzake ambao bado hawajafikishwa mahakamani, walikula njama kusaidia na kuwezesha kutenda kwa vitendo vya kigaidi.
Katika mashitaka mengine Swalehe anatuhumiwa kuchochea na kuwezesha watu kutenda vitendo vya kigaidi, ambapo ilidaiwa katika tarehe hizo hizo  alikuwa akiwasiliana na watu nje ya Tanzania.
Inadaiwa alifanya mawasiliano hayo ili kupata misaada ya vifaa, fedha na ujuzi wa kulipua mabomu sehemu tofauti tofauti katika Jamhuri ya Kenya kwa lengo la kuwadhuru watu wa Kenya jambo ambalo ni kinyume cha Sheria ya Ugaidi.
Mshitakiwa hakutakiwa kujibu mashitaka kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo isipokuwa Mahakama Kuu.

Hata hivyo mshitakiwa alihoji kwanini katika hati ya mashitaka ya kwanza ilieleza mtu aliyewasiliana naye lakini hati hiyo aliyosomewa leo (jana) haina jina la mtu.
Hakimu Mchauru alisema kesi ya awali ilifutwa na hiyo ni kesi nyingine hivyo aliahirisha shauri hilo hadi Februari 2 mwaka huu itakapotajwa tena.
Awali, kesi hiyo ilifutwa kutokana na kutokuwepo kwa kibali cha Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) hata hivyo upande wa Jamhuri uliwasilisha kibali hicho na kufungua mashitaka hayo upya.

No comments: