Mkutano wa 18 wa Bunge unatarajiwa kuanza leo mjini
Dodoma, lakini hoja nzito ambazo zinatarajia kuibua mijadala mizito ni Muswada
wa Marekebisho ya Sheria mbalimbali wa mwaka 2014 na taarifa za Mdhibiti na Mkaguzi
Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Jumla
ya miswada mitatu itawasilishwa kwenye mkutano huo, lakini tayari kuna dalili
kuwa muswada wa marekebisho ya sheria mbalimbali, ambao unagusa kuundwa kwa
Mahakama ya Kadhi, unaweza kuibua mjadala mzito bungeni, kutokana na suala hilo kila linapoibuka
wabunge wamekuwa wanagawanyika.
Huu
utakuwa ni mkutano wa kwanza wa Bunge, bila kuwepo kwa vigogo ambao
wameondolewa au kujiuzulu, kutokana na kashfa ya Tegeta Escrow. Vigogo hao ni
Mwanasheria Mkuu wa zamani, Jaji Frederick Werema, aliyekuwa Waziri wa Ardhi,
Nyumba na Makazi, Profesa Anna Tibaijuka na Waziri wa Madini na Nishati,
Profesa Sospeter Muhongo.
Kwa
mujibu wa taarifa iliyotolewa na Idara ya Habari, Elimu kwa Umma na Uhusiano wa
Kimataifa ya Bunge hilo, katika mkutano huo moja ya shughuli ambazo
zitafanywa na Bunge ni kujadili taarifa
za CAG zilizowasilishwa katika Mkutano wa 15.
Miongoni
mwa madudu ambayo Ripoti ya CAG ilibaini serikalini ni malipo ya mishahara hewa, kupotea kwa
stakabadhi kwenye halmashauri, uwindaji haramu unavyoongezeka na kandarasi tata
ndani ya Mamlaka ya Bandari nchini (TPA).
Wenyeviti
wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali
(PAC) na Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), watawasilisha
ripoti zao na serikali itajibu taarifa hizo, ambazo ni hesabu za mwaka 2012/13.
Pia,
katika mkutano huo, Kamati za Bunge nazo zitapewa nafasi ya kuwasilisha taarifa
za mwaka za shughuli za Kamati; na zitapangiwa muda wa kujadiliwa, kwa kadri
Spika atakavyoelekeza.
Hali
kadhalika, Kamati Teule ya Bunge iliyoundwa kuchunguza na kuchambua Sera
mbalimbali zinazohusu masuala ya ardhi, kilimo, mifugo maji na uwekezaji ili
kubaini kasoro zilizomo katika matumizi ya ardhi, itapewa nafasi ya kuwasilisha
taarifa yake, na taarifa hiyo itajadiliwa bungeni hapo.
Taarifa
hiyo ya Bunge ilisema miongoni mwa shughuli za leo bungeni ni kuapishwa kwa
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George
Masaju ambaye amejaza nafasi ya Jaji Werema.
Taarifa
hiyo ilitaja miswada itakayowasilishwa na kupitishwa katika vikao vya Bunge ni
Muswada wa Sheria ya Usimamizi wa Kodi wa Mwaka 2014 ambao utapigiwa kura tu,
Muswada wa Muswada wa Sheria ya Takwimu wa mwaka 2013 na Muswada wa Marekebisho
ya Sheria mbalimbali Namba 2 wa mwaka 2014.
Wakati
huo huo, Jukwaa la Wakristo limetoa
tamko ambalo linaishauri Serikali kuuondoa bungeni Muswada huo wa Marekebisho
ya Sheria mbalimbali kwa kile linachodai kuwa ni kuepusha kuvunja misingi ya
taifa, ambalo halina ubaguzi na lisilo na dini yoyote.
Muswada
unaopingwa na jukwaa hilo ni ule ambao unapendekeza, pamoja na mambo mengine,
marekebisho ya Sheria ya tamko la Sheria za Kiislamu la mwaka 1964, ambao
unapendekeza kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi.
Tamko
hilo lilitolewa jijini Dar es Salaam jana kwenye taarifa iliyosainiwa na
viongozi wa Jukwaa hilo, ambao ni Askofu Dk Alex Malasusa wa Jumuiya ya
Kikiristo Tanzania (CCT) , Askofu
Tarcisius Ngalalekumtwa wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) na Askofu Daniel Awet kutoka Umoja wa Makanisa ya Pentekoste (CPCT) baada
ya mkutano uliowakutanisha Januari 20 mwaka huu.
Kwenye
tamko hilo, viongozi hao walieleza kuwa mapendekezo ya kurekebisha Sheria ya
tamko la Sheria za Kiislamu ni mapendekezo makubwa, yatakayokuwa na athari
kubwa na nzito, yakihoji msingi wa dola ya Tanzania kama dola isiyokuwa ya
kidini.
Tamko
hilo lilieleza kuwa kwa sababu hiyo, mapendekezo hayo yanaibua mambo mazito ya
kikatiba, ambayo hayawezi kuamuliwa na muswada huo.
Tamko
hilo lilibainisha kuwa sababu
zilizowezesha kufutwa kwa mahakama hizo mwaka 1963, ilikuwa kujenga umoja wa
kitaifa, kuondoa ubaguzi katika mfumo wa kisheria na utoaji haki sawa, jambo
ambalo bado ni halali na la msingi kwa
sasa.
" Kwa
sababu hiyo, kwa heshima kubwa, tunashauri
kwamba Serikali iondoe Muswada huu bungeni ili kuepusha kuvunja misingi
ya Taifa hili kama taifa lisilo la kibaguzi na lisilofungamana na dini.
Katika
tamko hilo, viongozi hao walisema kuwa, masuala yanayohusu imani za dini na
kujiingiza kwa Serikali katika masuala yanayohusu imani hizo, yanahitaji
mjadala mpana na maridhiano ya kitaifa.
No comments:
Post a Comment