MAMA ANYONGA WATOTO WAKE WAWILI HADI KUFA

Jeshi la Polisi mkoani  Tabora linamshikilia mama mkazi wa kata ya Chemchem Manispaa ya Tabora, Zuhura Masudi (pichani) mwenye umri wa miaka 25, kwa kosa la kuwanyonga watoto wake wawili hadi kufa.

Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Tabora, Juma Bwire alithibitisha kutokea kwa mauaji hayo na kusema  tukio hilo lilitokea Januari 25 mwaka huu majira ya saa moja jioni maeneo ya Chechem Manispaa ya Tabora.
Alitaja marehemu hao kuwa ni Mwamvua Mrisho mwenye umri wa  miaka minne  na mwingine aliyetambulika kwa jina moja la Sudi, anayekadiriwa kuwa na umri wa miezi minne.
Alisema kwamba baada ya mama huyo kufanya mauaji hayo, aliwaviringisha katika mifuko ya sandarusi, kisha kuwafukia chini, mmoja sebuleni na mwingine chumbani kwake.
Kamanda Bwire alisema tayari mama huyo na baba yake mzazi, Shabani Ramadhani (75) wanashikiliwa na polisi kwa mahojiano zaidi, kwa kuwa inadaiwa kwamba kulikuwa na ugomvi wa kugombea nyumba, kati ya mama huyo na Shabani Ramadhani.
Alisema huenda ugomvi huo wa nyumba, ndiyo chanzo cha mama huyo kuamua kuchukua uamuzi mgumu kama huo wa kuua wanawe.
Hata hivyo, Bwire alisema jeshi hilo linaendelea kufanya uchunguzi zaidi ili kuweza kubaini chanzo halisi cha vifo hivyo.
Alisema kwamba baada ya uchunguzi kukamilika, watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.
Kutoka Mpwapwa mwandishi anaripoti kuwa mtoto mwenye umri wa mwaka moja na miezi minne, amelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma akiwa na hali mbaya baada ya kupigwa na mchi kichwani na baba yake mzazi.
Mganga Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa, Saidi Mawji alisema mtoto huyo,  Yadiko Chigoda amepata jeraha kichwani na sasa anaendelea kupatiwa matibabu na uchunguzi zaidi.
“Ni kweli tumempokea mtoto huyo akiwa na mama yake na ndugu zake wengine waliomsindikiza, ameumia sana kichwani lakini bado anaendelea na tiba na uchunguzi zaidi kwenye fuvu la kichwa maana inaonesha kama limepasuka,” alisema.
Pia, Dk Mawji alisema wanafanya mpango wa kumhamishia mtoto huyo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma kwa matibabu zaidi.
Akizungumza katika wodi  namba saba katika hospitali hiyo, mama mzazi wa mtoto huyo, Caroline Mnyawami (32) ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Mingui  Kata ya Lumuma, alisema siku ya tukio majira ya saa nne mume wake, Fabian Chigoda alikuwa akimpiga kaka yake na ndipo akajaribu kuamulia ugomvi huo.
Alidai  alipojaribu kumnyang’anya mumewe fimbo, aliyokuwa akimpigia kaka yake, ndipo mumewe aliamua kuchukua mchi wa kinu na kumrushia kichwani, ambapo alikwepa na kisha mchi huo kumgonga mtoto, aliyekuwa amembeba mgongoni.
Baada ya mwanaume huyo kuona amempiga mtoto, aliamua kukimbia na mpaka sasa hajulikani alipo.
Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Mingui, Mwingwa Udoba, alithibitisha kutokea kwa  tukio hilo na kusema chanzo cha ugomvi ni masuala ya kifamilia. “Bado tunaendelea kumtafuta, kwani alikimbia baada ya tukio na akipatikana atafikishwa kwenye mikono ya sheria,” alisema.

No comments: