SHILINGI TRILIONI MOJA KUTUMIKA KUPUNGUZA FOLENI DAR

Wizara ya Ujenzi imezindua miradi  ya ujenzi wa barabara za kupunguza msongamano wa magari jijini Dar es Salaam,  zitakazogharimu Sh trilioni moja.

Akizindua miradi huo, Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli  alieleza kuwa miradi hiyo inajumuisha barabara zenye jumla ya  kilometa 55.2  na kwamba baada ya miaka mitatu, tatizo  la msongamano wa magari jijini litakuwa historia.
Barabara zilizozinduliwa ni ile ya Msewe – Baruti  hadi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam yenye urefu wa Km 2.6, Kigogo -Tabata km 1.6, Mbezi Mwisho- Goba hadi Tangibovu km 9, External - Kilungule km 3, Wazo mpaka Goba km 20 na  Mbezi Mwisho mpaka Kinyerezi km 14.
Katika ziara hiyo,  Dk Magufuli aliongozana na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, wabunge wa maeneo husika na wananchi wa maeneo hayo.
Magufuli aliwataka wakandarasi kukamilisha miradi kwa muda uliopangwa na kutaka suala la msongamano wa magari, hususan ujenzi wa barabara hizo, uangaliwe kwa jicho la huruma kwa wabunge wa mkoa huo kuungana katika kutetea bungeni.
Alisema serikali ina uwezo kuwalipa wakandarasi wote  na kuwataka waendelee na kazi kwa kuwa  wiki iliyopita wamepata fedha kutoka Wizara ya Fedha  na wataendelea kulipa wakandarasi kwa awamu.
“Miradi hii inagharimu Sh trilioni moja na baada ya miaka mitatu suala la msongamano litakuwa historia… tulichelewa kuanza kujenga barabara hizo, lakini tumeanza na tutakamilisha,“alisema.
Dk Magufuli alieleza kuwa katika kuhakikisha misongamano inakuwa historia, lazima wakazi wote kuungana na kuzingatia sheria kwa kuacha kufanya biashara katika barabara za pembeni, ikiwa ni pamoja na kila mmoja kuwa mlinzi wa barabara. 
“Kwa mfano, barabara za mradi wa mabasi yaendayo kasi zitakazokamilika mwezi Machi mwaka huu na kuanza kutumika, sasa zinafanywa ni soko kwa wafanyabiashara, hilo ni kosa,” alisema.
Magufuli alimtaka mkuu wa mkoa na viongozi wa siasa, kuzingatia sheria kwa kuondoa wauza matofali, gereji, mitumba na wengineo.
Wakati wa uzinduzi wa barabara ya Msewe, Magufuli aliahidi kujenga ukuta wa shule ya msingi Msewe huku Mbunge wa Ubungo, John Mnyika alichangia madawati yenye thamani ya Sh milioni 10  kutoka  Mfuko wa Jimbo. Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Ramadhani Madabida aliahidi CCM itachangia Sh milioni tano kwa ajili ya madawati shuleni hapo.
Awali, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini (Tanroads), Patrick Mfugale  alisema barabra zote hizo, zinasimamiwa na Tanroads kwa km 55.2 na barabara za urefu wa km 27.2 zimeishaanza kujengwa.
Alisema changamoto waliyonayo katika ujenzi wa barabara hizo ni malipo ya makandarasi kuchelewa, jambo linalosababisha ujenzi wa barabara hizo kuchelewa kukamilika kwa muda uliopangwa.

No comments: