KIVUKO CHA MV MAGOGONI CHAWEKA ROHO JUU ABIRIA

Baadhi ya wakazi wa Kigamboni wanaotumia kivuko cha Mv Magogoni wameiomba serikali kukifanyia marekebisho kivuko hicho ambacho kimekuwa kikipata hitilafu mara kwa mara na kutishia maisha ya abiria wake.

Wakizungumza na mwandishi wananchi hao walisema kivuko hicho kimekuwa na hitilafu kwa muda mrefu kabla hata ya kivuko cha Mv Kigamboni kwenda kufanyiwa matengenezo.
Walisema kwa sasa ni jambo la kawaida mtu kupanda kivuko hicho na baada ya muda kupoteza uelekeo, hali ambayo inawafanya wakazi wengi wa Kigamboni kukikwepa na kusubiria kivuko kidogo.
Akizungumzia tatizo hilo Mwanamisi Juma, mkazi wa Kigamboni alisema: “Kivuko hiki kimekuwa na hitilafu ya mara kwa mara hivyo mimi nikifika hapa nikikuta kivuko kidogo hakipo hata kama nina haraka kiasi gani sipandi hicho kikubwa hadi kidogo kitakaporudi kupakia kwa sababu naogopa kuhatarisha maisha yangu na pia sijui kuogelea hatari itakapotokea,” alisema.
Naye Salim Hamad, mkazi wa Kigamboni alisema anaogopa kivuko hicho na haamini kwamba kina usalama kwa sababu hata vifaa vya uokoaji ni vya muda mrefu na haamini kama ni vizima na vina uwezo wa kufanya kazi endapo hitilafu itatokea.
“Mimi ni muda mrefu sipandi kivuko hicho na woga ulizidi pale Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli aliposema Kivuko cha Mv Magogoni ni kibovu zaidi ya Mv Kigamboni wakati kikifanyiwa matengenezo na aliahidi ndani ya mwezi kivuko kidogo kikirudi angekiondoa na hicho kikubwa lakini kinachoshangaza hadi leo kipo kinafanya kazi na kuendelea kukwama kila siku,” alisema.
Mara kadhaa mwandishi ameshuhudia wananchi wanaotumia kivuko hicho wakisuasua kukipanda na kusubiri kivuko kidogo.
Mwandishi alimtafuta Dk Magufuli jana kuzungumzia suala hilo, lakini hakupatikana.
Hata hivyo, Septemba mwaka jana wakati alipotembelea eneo kilipofanyiwa matengenezo kivuko cha Mv Kigamboni, yaliyokuwa yanafanywa na  Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania(JWTZ) Kamandi ya Maji, Dk Magufuli alisema “Nawaahidi kivuko cha Mv Kigamboni kikirudi mjipange tena kwa sababu tutawaletea Kivuko cha Mv Magogoni nacho mkifanyie matengenezo kwa kuwa muda wake umewadia. Nataka hata kama kuna kushindanishwa nyie ndiyo mshinde kwa kuwa mmefanya kazi nzuri na pia nyie siyo wezi” .
Alisema, “kama kivuko hicho kingetengenezwa huko nje usalama na ubora wake ungekuwa wa mashaka kwa sababu hata wasingepata muda wa kukitembelea na kukagua kazi inavyoendelea kama tunavyofanya sasa na hata tungetuma watu  pengine nao wangeongea nao vizuri”.

No comments: