Chuo cha Elimu ya
Biashara (CBE) kimekusanya zaidi ya Sh milioni 540.8 kwa ajili ya kufanya
upanuzi wa chuo hicho na kuboresha miundombinu, ikiwemo kujenga vyumba vya
mihadhara.
Akizungumza juzi Dar es
Salaam katika hafla ya kuchangisha fedha hizo, Mkuu wa Chuo hicho Profesa
Emmanuel Mjema alisema wamekuwa wakikabiliwa na changamoto mbalimbali kwa muda
mrefu na hivyo kuamua kufanya utaratibu huo, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya
miaka 50 ya chuo hicho.
Alisema chuo hicho
ambacho kililenga kukusanya Sh bilioni moja, kina uhaba wa hosteli za wanafunzi
ambapo hosteli iliyopo ina uwezo wa kuchukua wanafunzi 250 tu, hivyo fedha hizo
zitatumika kufanya mambo mbalimbali ikiwemo utafiti.
Mapema
Mwenyekiti wa Bodi ya Uongozi wa Chuo hicho, Profesa Mathew Luhanga alisema
chuo kimejitahidi kuwekeza katika kununua maeneo lakini changamoto kubwa
waliyonayo ni fedha za kuendeleza maeneo hayo.
Alisema CBE
ilianzishwa mwaka 1965 ikiwa na wanafunzi 25 na ikitoa kozi moja lakini hadi
kufikia mwaka huu wa masomo ilikuwa na wanafunzi 14,000 ikitoa kozi sita.
Alisema
katika miaka 50 ya chuo hicho wanajivunia mambo mbalimbali katika jamii ikiwemo
kutoa wataalamu zaidi ya 100,000 katika fani mbalimbali ambapo pia wametoa mafunzo
kwa wajasiriamali zaidi ya 5,000.
Katika hafla
hiyo, Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd ambae alikuwa mgeni
rasmi alichangia Sh milioni tatu na kuahidi kwamba serikali itaendelea kutoa
kipaumbele katika sekta ya elimu.
No comments:
Post a Comment