SERIKALI YABEBA MADENI YOTE YA ATCL


Serikali imekubali kuchukua madeni yote ya Kampuni ya Ndege ya Tanzania (ATCL) na kuyalipa, baada ya uhakiki ili kutoa fursa kwa shirika hilo kuanza biashara.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Monica Mwamunyange, alisema hayo mbele ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) na kuongeza kuwa kinachofuatia ni kuunda upya shirika hilo.
“Shirika hilo litaundwa upya, ikiwa ni pamoja na kumtafuta kiongozi wake kwani Mkurugenzi wa sasa atastaafu mwezi ujao, ikiwa ni pamoja na kupunguza wafanyakazi na kubaki na nguvu kazi yenye tija, kwani kwa sasa tuna ndege moja lakini kuna wafanyakazi 140,” alisema.
Mbali na kuundwa upya kwa kampuni hiyo, Mwamunyange alisema Serikali inaendelea na mchakato wa kununua ndege mbili aina ya D8-Q400 kutoka kampuni ya Bombardier Canada, kwa gharama ya Dola za Marekani milioni 32.87 kwa kila moja.
Ndege hizo kwa mujibu wa Mwamunyange, zitanunuliwa kwa mkopo kutoka Benki ya Maendeleo ya Tanzania (TIB) na zitatumika kutoa huduma za usafiri wa anga kwa soko la ndani na kikanda.
Mbali na ndege hizo mpya, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL, Kapteni Milton Lazaro alisema kwa sasa Kampuni hiyo inamiliki ndege moja aina ya Dash 8-Q300 ambayo ina uwezo wa kubeba abiria 50.
Kwa mujibu wa Kapteni Lazaro, kwa sasa ndege hiyo ipo kwenye matengenezo kuanzia Oktoba 24, mwaka jana na inatarajiwa kukamilika Februari 2015, ila kwa sasa kampuni hiyo imekodisha ndege mbadala moja.
Akifafanua uchukuaji wa madeni hayo, Mwamunyange alisema  Serikali inafanya majadiliano na baadhi ya wadai wa kampuni hiyo, kuangalia uwezekano wa kuondoa riba ili kupunguza deni la msingi na gharama nyinginezo.
“Majadiliano na kampuni nne yamekamilika na wamekubali kuondoa gharama zinazofikia bilioni 17.13 katika deni lao,” alisema.
Mwamunyange pia alisema kampuni hiyo inakamilisha mpango wa biashara wa kampuni, utakaoonesha mahitaji ya ATCL kwa miaka mitano hadi kumi, utakaoainisha mahitaji ya rasilimali watu na kuwasilishwa serikalini.
Alisema mpango huo wa kibiashara ambao uko katika hatua za mwisho, pia utaonesha mwelekeo huku wakitarajia kushirikisha sekta binafsi. 
Alisema pia Serikali itaendelea kutafuta wawekezaji kwani awali baadhi ya kampuni za wawekezaji hazikuwa na sifa, na baadhi zilikuwa na masharti ambayo hayana manufaa kwa ATCL, huku zingine zikisita kuwekeza kutokana na deni kubwa la shirika hilo.
Alisema changamoto zingine zinazoikabili ATCL ni ukosefu wa vitendea kazi na wataalamu wa ndege ambao ni marubani na wahandisi.
Changamoto nyingine ni kutokuwa na mtaji wa kutosha  na madeni yanayoongezeka kutokana na riba ya wadai na kushuka kwa thamani ya shilingi kwa kuwa madeni mengi yapo katika fedha za kigeni,  ambapo hadi kufikia Desemba  2014 Shirika lilikuwa na madeni ya Sh bilioni 95.7.
Alisema baadhi ya wadai wamefikisha Shirika mahakamani na kutishia kuchukua rasilimali zake, ikiwemo Kampuni ya Leisure Tours and Holidays, Wellworth Hotel and Lodges,  Kunduchi Hotel and Resort na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).
Alisema kampuni hiyo pia inakabiliwa na changamoto ya idadi kubwa ya wafanyakazi, ikilinganishwa na rasilimali zilizopo na mikataba mibovu iliyosainiwa na viongozi wa kampuni waliokuwepo miaka ya nyuma ambayo haikuwa na tija na ATCL.
Mwenyekiti wa PAC, Kabwe Zitto alipongeza mikakati hiyo ya Serikali kuinua shirika hilo, lakini alitaka watumishi wa kamapuni na watendaji serikalini waliohusika katika mkataba wa kampuni ya Walls Trading Inc na ATCL, iliyosababisha Serikali kuingia gharama za mabilioni ya fedha, wapelekwe mahakamani.
Pia alimtaka Mwanasheria wa kampuni hiyo kuangalia uwezekano wa kupeleka mahakama kampuni hiyo, kutokana na kukiuka mkataba ili kudhihirisha umma kuwa nchi haiwezi kuingiwa na matapeli.
Akizungumzia suala hilo, Zitto alisema kampuni ya China Sonangol ambayo alikuwa mbia wa ATCL ilitafuta ndege ya kukodi ya Airbus 320 kutoka Liberia,  ambayo ilifanya kazi kwa miezi sita na kwenda nchini Mauritius kwa matengenezo Machi mwaka 2009 na kukamilika Novemba mwaka huo kwa Dola 3,000,000.
Alisema kutokana na mkataba, matengenezo yalitakiwa kufanywa na ATCL tofauti na mikataba ya kimataifa ambayo mwenye ndege ndiyo anatakiwa kutengeneza jambo ambalo liliilazimu Serikali kulipa huku ndege hiyo ikifanya kazi nchini Guinea.
Julai mwaka jana, Naibu Waziri wa Uchukuzi, Dk Charles Tizeba alisema ATCL ina mpango wa kununua ndege nyingine mbili, kwa mfumo wa kibiashara wa kukodi huku malipo ya ununuzi yakifanyika taratibu.
Ndege hizo aina ya D8 Q 400, zenye uwezo wa kubeba abiria 78 kila moja baada ya kununuliwa, zitaongeza wigo wa huduma za ATCL katika njia za Nairobi nchini Kenya, Kigali nchini Rwanda na nchini Uganda.
Kwa mujibu wa maelezo ya Dk Tizeba aliyoyatoa bungeni, ununuzi wa ndege hizo utafanyika baada ya kukamilika kwa taratibu za kisheria na kibiashara ambazo zinafuatwa.
Baada ya kukamilika kwa utekelezaji wa mpango huo, ambao utafanya ATCL kurusha ndege nne na kutoa huduma za ndani na katika nchi za Afrika Mashariki, Dk Tizeba alisema utafuata utekelezaji wa ununuzi wa ndege nyingine mbili.
“Kuna mpango wa kununua ndege mbili ndogo aina ya Y12E, kwa mkopo nafuu wa Exim Bank kutoka China kwa Serikali ya Tanzania, kila moja ina uwezo wa kubeba abiria 20,” alisema.
"Mbali na ndege hizo, pia Serikali kwa mujibu wa Dk Tizeba itanunua ndege mbili aina ya ERJ 170 na ERJ 190, zenye uwezo wa kubeba abiria 80 mpaka 100 kutoka nchini Brazil.
 “Ndege hizi zitanunuliwa kwa utaratibu wa mkopo kutoka Benki ya Maendeleo ya Brazil,” alisema Dk Tizeba na kusisitiza kuwa baada ya kupatikana kwa ndege hizo, ATCL itaanza kutumia njia zake za kimataifa kwa kuwa bado zipo.

No comments: