Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL)
imetangazwa kufilisika, kutokana na kutokuwa na mtaji baada ya mwekezaji,
Kampuni ya simu za mkononi ya Bharti Airtel, kushindwa kuwekeza kwa miaka 14.
Kutokana na hatua hiyo, Kamati ya Bunge
ya Kudumu ya Hesabu za Serikali (PAC) imeamua kupeleka suala hilo bungeni ili
kuweka mipango ya kimkakati kuifufua kampuni hiyo. Kwa kuanzia, Msajili wa
Hazina amepewa kazi ya kufanya tathmini ya kina.
Hayo yalibainika jana katika kikao cha
uongozi wa kampuni hiyo na kamati hiyo, inayoongozwa na Kabwe Zitto, iliyotaka
kufahamu maendeleo ya kampuni hiyo, ambayo kwa miaka mingi imekuwa ikikabiliwa na changamoto kadhaa
katika ushindani wa huduma za simu hususani katika siku za mkononi.
Umekuwepo pia mvutano mkali baina ya
Serikali na Kampuni ya simu za mkononi ya Bharti Airtel kuhusu hatima ya
asilimia 35 ya hisa, ambazo kampuni hiyo inamiliki ndani ya Kampuni ya TTCL.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo, Dk
Kamugisha Kazaura aliieleza Kamati ya
Bunge kuwa kutokana na hasara kubwa ya kiasi cha Sh bilioni 334.5 mpaka kufikia
mwaka 2013 na kushindwa kukopesheka huku ikibaki na mtaji hasi wa Sh bilioni
87.9, kwa sasa ni mufilisi.
Alisema hatua hiyo, inatokana na mbia
mwenye hisa kwa asilimia 35, kutofanya uwekezaji mkubwa tangu waingie ubia
mwaka 2001, jambo ambalo limesababisha pia uchakavu wa miundombinu na kupungua
kwa ubora wa huduma.
Kutokana na hatua hiyo ya kutokuwekeza,
kampuni hiyo ilimtaka mwekezaji huyo kuondoa umiliki alionao, ambapo Msajili wa Hazina, Lawrence
Mafuru alisema kampuni hiyo ya India,
ambayo ni Kampuni mama ya Airtel Tanzania, inataka ilipwe Sh bilioni 14 licha
ya kuwa haijawahi kuwekeza chochote ndani ya TTCL, kama ilivyo kwa watangulizi wake; Celtel Tanzania, Celtel
International na Zain.
Lakini, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano,
Sayansi na Teknolojia, Profesa Patrick Makungu alisema Baraza la Mawaziri
limeunda jopo la majadiliano na mwekezaji huyo, kuzungumzia gharama za kumlipa
ili kuondoka katika kampuni hiyo ya TTCL na hawana taarifa ya kiwango hicho cha
fedha kilichotajwa.
“Mitambo mingi ni chakavu, kutokana na
kutowekeza katika teknolojia za kisasa kwani kampuni nyingine za simu za
mkononi kila mwaka zimekuwa zikiwekeza dola milioni 100 kuboresha huduma,”
alisema.
Alisisitiza kuwa kwa mwaka 2012, mapato
ya kampuni hiyo yalikuwa Sh bilioni 92.4 lakini mwaka uliofuata yaliongezeka
kwa asilimia moja na kufikia Sh bilioni 93.6 baada ya jitihada mbalimbali
katika kukuza teknolojia.
Akizungumzia hasara ya kampuni hiyo,
alisema mwaka 2012 hasara ilikuwa Sh bilioni 20.8 na mwaka 2013 ilikuwa Sh
bilioni 16.2, jambo linalosababisha hali ya fedha kuwa mbaya na kushindwa
kukopesheka kutokana na serikali kushindwa kuwadhamini.
Alisema asilimia 50 ya miundombinu ya
kampuni hiyo ni chakavu huku wakitegemea mapato kwa kutumia wateja. Alitaka
serikali kuwafutia deni la Sh bilioni 76 wanazodaiwa baada ya kukopeshwa
serikali ilipouza hisa zake na kutumia kulipa wafanyakazi waliostaafu.
Dk Kazaura alisema uhaba wa fedha, pia
unasababishwa na madeni mengi kampuni hiyo inadai idara na taasisi ya serikali,
ambapo hadi kufikia Septemba 2014 walikuwa wakiidai Sh bilioni 3.2 na dola za
Marekani milioni mbili, hivyo waliomba
Hazina kusaidia kwa kukata taasisi na idara hizo moja kwa moja kwenye mafungu
yao.
Alisema licha ya changamoto hizo, bado
wanadaiwa na wazabuni, Mamlaka Mawasiliano Tanzania (TCRA) na taasisi nyingine
za kimataifa, jambo lililofanya TCRA kuwaagiza kulipa madeni hayo hadi Oktoba
31,mwaka jana, vinginevyo watafutiwa leseni .
Lakini, pia alisema wanaiomba serikali
kuangalia namna ya kuwaongezea mtaji kufikia dola milioni 711 ili kufufua
shirika, ikiwa ni pamoja na kuwamilikisha rasmi mkongo wa taifa wa mawasiliano,
ambao kwa sasa wanausimamia baada ya kukamilika kwa awamu mbili.
“Pia tunahitaji kurekebisha muundo wa
kampuni kutokana na kuwa na wafanyakazi wengi wanaofikia 1,550 na wengi wao
ambao ni asilimia 50 wana miaka zaidi ya 50
na elimu isiyozidi kidato cha nne, hivyo lazima kuchambua watakaoweza
kuendana na teknolojia na ikibidi wengine kuwapisha wenye uwezo,” alisema.
Waliomba serikali pia kuangalia suala la
taratibu na sheria za manunuzi ili
kusaidia ushindani wa kibiashara na kampuni nyingine za simu za mikononi,
ambazo ni binafsi na taratibu zake hazichukui muda mrefu.
Alizungumzia pia suala la gharama kubwa
za intaneti ya TTCL kuwa inatokana na ubora wake na uhakika kwa huduma
zinazotolewa huku akitaka wananchi kuwaunga mkono katika huduma hiyo.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Kabwe Zitto
alisema watapeleka bungeni suala hilo
ili litolewe maamuzi ya pamoja na
wabunge na kuweka mikakati ya kunusuru kampuni hiyo yenye kukabiliwa na
madeni, ukosefu wa mtaji pamoja na kufanya maamuzi ya kwa kuondoka kwa mwekezaji.
Alisema wamemtaka Msajili wa Hazina
kufanya tathmini ya majadiliano na kupeleka taarifa katika kamati hiyo siku ya
Ijumaa ili kutafuta njia ya kunusuru kampuni hiyo na kuhakikisha inafanya kazi
kwa faida na kushindana na kampuni nyingine.
Zitto alisema baadhi ya maamuzi
yaliyofanywa kwenye kampuni hiyo, ikiwemo leseni na masafa yake kutumiwa bure na kampuni ya
Celtel ambayo sasa ni Airtel na kufanya TTCL sasa wanatafuta upya.
“Kampuni kwa sasa imefilisika kutokana na
kuwa na mizania ya bilioni 157 ya ziada lazima maamuzi yafanyike na tathmini
kupelekwa bungeni ili yafanyike maamuzi sahihi,” alisema Zitto.
Februari 21, 2001, TTCL ilisaini mkataba
na Kampuni ya SMI/Detecon, ambayo ilinunua asilimia 35 ya hisa kwa Dola za
Marekani 120 milioni (Sh bilioni 198).
Hata hivyo, kiasi kilicholipwa ni Dola 65
milioni tu (Sh bilioni 107.3) kwa ahadi kwamba kiasi kilichosalia, kingelipwa
baada ya hesabu za TTCL kukaguliwa.
Baadaye MSI/Detecon ambao ulikuwa
ushirika wa Kampuni ya Mobile Systems International ya Uholanzi na Detecon ya
Ujerumani, ilitumia leseni ya biashara ya simu za mkononi iliyokuwa mali ya
TTCL, kuanzisha Celtel Tanzania.
Baada ya kuundwa kwa Celtel Tanzania,
TCCL walipewa umiliki wa asilimia 40 ya hisa, baada ya muda mfupi, hisa hizo
zilihamishiwa Hazina, hivyo kuiacha TTCL bila hisa wala biashara ya simu za
mkononi.
Katika mchakato huo, Celtel Tanzania
iliuzwa kwa Celtel International ambayo baadaye iliuzwa kwa Zain. Juni 2010,
Zain iliuzwa kwa Kampuni ya Bharti Airtel Limited ambayo ndiye mmiliki Airtel
Tanzania.
No comments:
Post a Comment