Askari wawili wa Jeshi la Polisi katika
Kituo cha Ikwiriri wilayani Rufiji mkoani Pwani, wameuawa baada ya kushambuliwa
kwa silaha na majambazi, waliovamia kituo hicho na kuiba silaha baada ya
kufanikisha mauaji.
Kutokana na tukio hilo, Jeshi la Polisi
liko katika msako mkali, huku Mkuu wa jeshi hilo, IGP, Ernest Mangu akitangaza
donge nono la Sh milioni 20 kwa watakaofanikisha kukamatwa kwa wahusika wa
tukio hilo na silaha.
Akizungumza na waandishi wa habari kwa
njia ya simu kutoka eneo la tukio, Ikwiriri, Kamanda wa Polisi mkoani Pwani,
Ulrich Matei alisema majambazi hao walitumia silaha kuwaua askari hao.
Kamanda Matei alisema kuwa tukio hilo
lilitokea majira ya saa 8 usiku katika kituo hicho cha Polisi cha Ikwiriri.
Aliwataja askari waliokufa kuwa ni mwenye
namba E 8732 Koplo Edgar Milinga na WP 5558 Konstebo Judith Timothy.
Alisema licha ya kufanya mauaji hayo, pia
majambazi hao yalipora silaha tano za moto aina mbalimbali, zikiwemo SMG 2, SAR
3 na risasi 60. Pia, walichukua mabomu mawili ya machozi.
Kamanda alisema kuwa pia watu hao,
waliharibu kwa kulipiga risasi gari la Polisi la kituo hicho lenye namba za usajili PT 1965.
Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Advera
Bulimba alisema tukio hilo la kusikitisha,
halitapita hivi hivi, bali jeshi limeelekeza nguvu zake huko kuhakikisha
wahusika wanakamatwa.
Alisema tayari Mkuu wa Jeshi ametangaza
dau la Sh milioni 20. Pia, alisema katika kuongeza kasi ya msako, Kamishna wa Operesheni na Mafunzo, Paul Chagonja akiwa na
timu ya makachero, yuko eneo la tukio kuhakikisha wahusika, kokote waliko,
wanasakwa na kutiwa mbaroni.
“Hili ni sawa na tukio la
kigaidi, Jeshi la Polisi litakabiliana na wahusika kokote waliko, lazima
wakamatwe. Kikubwa tunaomba ushirikiano wa wananchi, tunaamini wengi ni raia
wema na watalisaidia jeshi kufanikisha jukumu hilo la kukomesha uhalifu nchini,”
alisema Advera.
Aliwataka wananchi kuelewa Jeshi la Polisi liko imara, hivyo wasiwe na
hofu yoyote juu ya tukio hilo. Alisisitiza kuwa wahusika wote watadhibitiwa na
kushikishwa adabu.
No comments:
Post a Comment