JWTZ YAWAONYA WANAOVAMIA VIWANJA VYAKE


Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ),  limeonya wananchi wanaovamia maeneo yanayomilikiwa na jeshi,  kuacha tabia hiyo mara moja, kwani inahatarisha usalama wa maeneo ya kambi na maisha yao.

Akizungumza na  mwandishi ofisini kwake, msemaji wa JWTZ, Meja Joseph Masanja (pichani) alisema kumekuwa na ongezeko la uvamizi wa maeneo ya jeshi, unaofanywa na wananchi.
Alisema pamoja na kuwepo alama za mabango na mawe, yanayoonesha mipaka halisi ya maeneo ya jeshi na maeneo yanayoruhusiwa wananchi kuishi, wananchi wamekuwa wakaidi na kuendelea kufanya uvamizi na kuendesha shughuli zao za makazi.
“Maeneo yote yanayomilikiwa na Jeshi, yamewekwa mipaka inayoonekana ya mawe  na mabango makubwa ya chuma kuashiria hapa ni eneo linalomilikiwa na jeshi. Hata hivyo wananchi wamekuwa wakikaidi na kuendelea na shughuli zao kinyume na sheria,” alisema Meja Masanja.
Aliongeza kuwa umbali halisi wa eneo ambalo wananchi wanaruhusiwa kuishi na kuendesha shughuli zao za maisha ni kuanzia mita 500 kutoka mpaka wa jeshi ulipoishia.
“Ni kweli kuna baadhi ya maeneo wananchi wanaishi karibu na maeneo ya jeshi, lakini kuna mipaka yake na umbali unaoruhusiwa kisheria. Umbali huo ni kuanzia mita 500 kutoka pale mpaka wa Jeshi ulipoishia,” alisema Meja Masanja.
Akitoa ufafanuzi wa taarifa iliyotolewa na vyombo vya habari kuhusu mgogoro wa wananchi waliovamia eneo la jeshi katika kijiji cha Tondoroni mkoa wa Pwani eneo la Kisarawe, alisema mgogoro huo ni wa muda mrefu na eneo hilo ni la jeshi.
“Eneo hilo linamilikiwa na jeshi na wananchi waliokuwa wanaishi pale walishafanyiwa tathmini na kulipwa fidia zao na kuamriwa wahame. Walipewa muda wa kufanya hivyo lakini hawakuweza kuondoka hivyo jeshi limechukua hatua ya kuwaondoa kwa kufuata taratibu zote na kuzingatia haki za kibinadamu,” alisema Masanja.
Aidha aliongeza kuwa kwa wale wananchi wanaodai hawajalipwa fidia za kuhama ni waongo na taarifa hizo sio za kweli, kwani kila mtu alishalipwa madai yake.
 “Kila mtu alishalipwa madai yake, bali kwa wale wanaodai hawajalipwa ni wageni waliorubuniwa na kuuziwa maeneo kiholela bila kufuata utaratibu, lakini wahusika wa maeneo yale yote walishalipwa sasa wao walichofanya wakahama na kuyauza maeneo yale kwa watu wengine. Jeshi haliwezi kulipa eneo moja mara mbili,” alisema Meja Masanja
Hata hivyo, jeshi linatoa tahadhari kwa wananchi wanaofanya uvamizi huo kwa kuwa maeneo ya jeshi sio salama kwa maisha ya wananchi, kwani kuna matumizi ya risasi za moto wakati wa mazoezi na zana zingine za kijeshi, ambazo zinaweza kuhatarisha usalama wao.

No comments: