Aliyejifanya Askari Polisi wa Usalama Barabarani,
James Hassan (54) amehukumiwa kifungo cha miaka sita jela baada ya kupatikana
na hatia ya kukutwa na sare za Polisi na kujifanya mtumishi wa jeshi hilo.
Aidha, adhabu hiyo ilitokana
na makosa mawili ambapo mshitakiwa huyo atatakiwa kutumikia kifungo cha miaka
mitatu mitatu kwa kila kosa.
Akisoma hukumu hiyo jana,
Hakimu Mkazi Mwandamizi, Hassan Juma wa Mahakama ya Wilaya ya Ilala, alisema
kwamba ametoa adhabu hiyo ambayo haitaenda kwa pamoja, kutokana na mshitakiwa
huyo kuwa ni mkosefu mzoefu.
Pia alisema kwamba mahakama
hiyo imemtia hatiani kupitia kwa mashahidi watatu wa upande wa mashitaka
walioithibitishia mahakama bila ya kuacha shaka.
Kabla ya hukumu, mshitakiwa
huyo alidai kwamba kwa kuwa mahakama imemwona kuwa ana hatia, yeye hakufanya
kosa hilo na hata ikiwezekana mahakama imuachie huru.
Hata hivyo, mahakama hiyo
ilitupilia mbali maombi hayo na badala yake alihukumiwa kifungo hicho.
Wakili wa serikali, Florida
Wenuslaus alidai kuwa mshitakiwa apewe adhabu iwe fundisho kwa wengine.
Katika kumbukumbu za makosa
ya nyuma ya mshitakiwa, ilibainika kwamba mshitakiwa huyo alihukumiwa kifungo
cha miaka 30 jela kwa kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha, katika mahakama ya
Wilaya ya Isanga, Dodoma na kufungwa katika gereza la Isanga mkoani humo.
Pia mshitakiwa huyo
alihukumiwa kifungo cha miaka sita jela kwa kosa la kukutwa na sare za Jeshi la
Polisi.
Katika barua iliyoandikwa na Mkuu wa Gereza la
Keko kwenda kwa Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, iliithibitishia mahakama
kwamba mshitakiwa huyo alikuwa na kesi namba 32 ya mwaka 2004 na kwamba
mshitakiwa alijiandikisha kwa jina la Ally Kinanda.
Pia barua hiyo ilieleza kuwa Hassan alitoroka
akiwa chini ya uangalizi wa jeshi hilo na kwamba asipatiwe dhamana baada ya
kukamatwa na kufikishwa katika mahakamana hiyo, kwa kuwa mshitakiwa alikana
kuhusika na tuhuma hizo na kueleza kuwa watafuata taratibu zote kuchukua alama
za vidole ili kuthibitisha kabla ya kupatiwa dhamana.
Ilidaiwa kwamba mshitakiwa alitenda kosa hilo
Agosti 14, 2014 maeneo ya Kinyerezi mnara wa Voda akijifanya kwamba ni askari
polisi wa Usalama barabarani.
No comments:
Post a Comment