ILALA YAANDIKISHA WATOTO 23,113 DARASA LA KWANZA NA LA AWALI

Halmashauri ya Manispaa ya Ilala imeshaandikisha wanafunzi  23,113 wa awali na darasa la kwanza kwa ajili ya kuanza masomo katika shule mbalimbali za manispaa hiyo.

Ofisa Habari wa Manispaa hiyo, David Langa alisema kati ya wanafunzi hao walioandikishwa, 18,253 ni wa darasa la kwanza na 4,860 ni wa awali.
Alisema  uandikishaji unaendelea vizuri hadi sasa, ingawa changamoto kubwa ni wazazi kwenda kuwaandikisha watoto wao shule za mbali, tofauti na maeneo wanayoishi.
“Tunachofanya ni kuwaelimisha kwamba shule zote ni sawa, hivyo hakuna haja ya mzazi wa Gongo la Mboto kuja kumuandikisha mtoto wake shule za Posta Mpya  katikati ya jiji wakati huko Gongo la Mboto pia shule zipo,” alisema.
Aidha, Langa alisema manispaa hiyo imefanikiwa kuboresha usafi wa mazingira katika shule za msingi baada ya kuanzisha mashindano endelevu ya utunzaji na uboreshaji wa mazingira, ambao hufanyika Aprili 15 kila mwaka.
“Kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa elimu, Manispaa imeweza kupiga hatua kubwa katika kuleta mabadiliko katika sekta ya elimu ambapo uwiano wa kitabu kwa mwanafunzi umepungua kutoka 1:4 mwaka 2013 hadi kufikia 1:3 mwaka 2014” alisema
Pia, alisema wamekuwa wawashirikisha wadau na wafadhili mbalimbali wakiwemo wa Elimu, mashirika, watu binafsi na Taasisi katika kupunguza uhaba wa madawati.

No comments: