MAGEREZA BADO WAMSAKA MTUHUMIWA WA MAUAJI ALIYETOROKA

Mkuu  wa Magereza Mkoa wa Dar es Salaam, Joel Bukuku amesema  jeshi hilo bado linaendelea kuwachunguza askari wawili waliokuwa wakimlinda mshitakiwa Salim  Marwa (pichani) aliyetoroka akisubiri kupatiwa matibabu hospitali ya Temeke.

Marwa ni mshtakiwa wa kwanza katika kesi ya mauaji ya raia wa Ghana, Joseph Opong.
Bukuku alisema hayo jana Dar es Salaam wakati akizungumza na HabariLeo na kuongeza kuwa mshtakiwa huyo ataendelea kutafutwa siku zote hadi atakapopatikana.
Alisema kwa mujibu wa sheria za Idara ya jeshi hilo, askari hao wanachunguzwa kisha kufunguliwa mashtaka pindi itakapobainika kuwa walihusika kwa lolote hadi kutoroka kwa mshtakiwa huyo.
Bukuku alisema pindi askari hao watakapobainika kuhusika kwa uzembe kwa kosa lolote kuhusu utoro huo watapewa kupewa adhabu kwa mujibu wa taratibu za Jeshi hilo.
Mshtakiwa huyo alitoroka Jumatatu ya wiki iliyopita usiku majira ya saa 6:00  akiwa chini ya ulinzi akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Temeke,Dar es Salaam akiwa na askari magereza wawili.
Marwa anashtakiwa kwa mauaji ya kikatili ya raia wa Ghana, Joseph Opong huko Bagamoyo mwaka 2010 ambapo alikuwa rumande kipindi hicho katika mahabusu ya Keko hapa Dar es Salaam kabla ya kufikishwa hospitalini kwa matibabu.
Mbali na Marwa, ambaye inadaiwa kusoma kozi ya urubani, mshtakiwa mwingine katika kesi hiyo ni Peter Charles Mayalla, ambaye ni mshtakiwa wa pili katika kesi hiyo.
Inadaiwa  kuwa Septemba 10, 2010, washtakiwa hao walimuua kwa makusudi Opong, kwa kumkatakata sehemu mbalimbali za mwili, baada ya kumlewesha kwa dawa za kulevya na kisha kwenda kumzika katika msitu wa Kaole.

No comments: