AMUUA MDAI WAKE KWA KUKERWA KUDAIWA 80,000/-

Mwanamke mmoja Caseline Mzee (75) mkazi wa kijiji cha Guta Wilayani Bunda, Mkoani Mara, ameuawa kwa kupigwa na kitu kizito kichwani na kunyongwa shingo na kisha mwili wake kutupwa ndani ya mto ukiwa umefungiwa mawe mazito ili usielee.

Mwanaume anayedaiwa kufanya mauaji hayo ametambuliwa kwa jina la Malaki Malongo (56) mkazi wa kijiji hicho, ambaye inadaiwa alimuua kinyama mwanamke huyo baada ya kudaiwa Sh. 80,000, zilizotokana na marehemu huyomama huyo kumtibu mke wake ugonjwa wa kifafa.
Kamanda wa polisi Mkoani Mara, Philpo Kalangi,  alithibitisha jana kutokea kwa tukio hilo lililotokea Desemba 31 mwaka jana  saa 2:00 usiku katika kijiji cha Guta, ambapo mwili wa marehemu ulipatikana juzi ndani ya mto huo ukiwa umeharibika vibaya.
Kamanda Kalangi alisema chanzo cha mtuhumiwa huyo kumuua mwanamke huyo ni pale alipodaiwa Sh 80,000 ambazo ulikuwa ujira wake baada ya kumtibu mke wake ugonjwa wa kifafa.
Alisema marehemu alikuwa akiishi nyumbani kwa mwanaume kwa kipindi kirefu baada ya kutoka Wilayani Serengeti, ambapo alitumia fursa hiyo kumtibu mke wa mwenyeji wake ugonjwa wa kifafa kwa makubaliano ya kulipwa Sh 80,000.
Alisema siku ya tukio mwanaume huyo alifika nyumbani hapo akiwa amelewa pombe na ndipo alipoingia ndani na kuanza kumshambulia kwa kipigo mwanamke huyo, huku akimwambia kwamba ni kwanini amekuwa akimdai hizo fedha mara kwa mara.
Binti wa mwanaume huyo mwenye umri wa miaka 13 aliyeshuhudia mauaji hayo alisema baba yake alimpiga na kitu kizito kichwani mwanamke huyo na kisha akamnyonga shingo hadi akakata roho.
Alisema baada ya mauaji hayo baba yake alichukua mwili wa marehemu na kuuweka kwenye gunia la sandurusi na kisha akamlazimisha mke wake ili amsaidie kuubeba na kwamba walikwenda kuutupa ndani ya mto Nyandago ulioko mita 450 kutoka nyumbani kwao.
“Alimpiga na kitu kizito kichwani na kumnyoga shingo akitumia mikono, huyo mama alilia na kutoa sauti mara nne na kisha akanyamaza kabisa…..baba alichukuwa gunia na kuuweka mwili wa marehemu na kuufunga na ndipo akamlazimisha mama amsaidie kuubeba wakaenda kuutupa kwenye mto Nyandago” alisema.
Binti huyo alisema  baba yake wakati akifanya mauaji hayo, alimtishia kwamba kamwe asithubutu kumwambia mtu yeyote juu ya tukio hilo na kwamba kama atatoa siri hiyo atamuua kama alivyomua mwanamke huyo.
“Aliniambia nikimwambia mtu yeyote na mimi ataniua kama alivyomua, nilinyamaza hadi juzi ndipo tukasikia yowe kwenye eneo la tukio na baba naye akaenda huko na ndipo wananchi wakamkamata na kuita polisi” alisema.
Kamanda Kalangi alisema kuwa mwili wa marehemu huyo ulipatikana juzi saa 8:00 mchana, baada ya wananchi kupita katika eneo hilo na kuukuta ukielea huku ukiwa umeharibika vibaya na ukiwa ndani ya gunia na umefungiwa mawe mazito.
Alisema kuwa wananchi hao walitoa taarifa polisi waliofika katika eneo la tukio wakiongozwa na afisa upelelezi wa makosa ya jinai Wilayani Bunda, Gofrey Munguwajuna na kwamba daktari aliyeufanyia uchunguzi mwili huyo alithibitisha kwamba kabla ya kuuawa alipigwa na kitu kizito kichwani na kunyongwa shingo lake.
Alisema kuwa jeshi la polisi Wilayani Bunda linamshikilia mwanaume huyo, pamoja na mke wake aitwaye Taabu Masalo (49), ambapo pia wanamuhoji mtoto huyo ambaye ndiye aliyeshuhudia baba yake akifanya mauaji hayo ya kinyama.
Aliongeza kuwa baada ya mtuhumiwa huyo kuhojiwa na polisi alikiri kumuua mwanamke huyo na kwamba chanzo ni kutokana na kudaiwa shilingi 80,000 mara kwa mara.
Alisema kuwa bado polisi wanaendelea na upelelezi juu ya tukio hilo na ukikamilika watamfikisha mahakamani mtuhumiwa huyo.
Wilaya ya Bunda imekuwa ikikumbwa na matukio ya kikatili ya mara kwa mara ambapo  hivi karibuni wana ndoa wawili akiwemo mlemavu wa macho, wakazi wa kijiji cha Mcharo, waliuawa kwa kukatwa katwa mapanga na kuchukuliwa sehemu ya viungo vyao kwa kile kinachodaiwa ni mgogoro wa ardhi ekari moja.

No comments: