WATOTO 53 WAONDOKA LEO KWENDA INDIA KWA MATIBABU

Watoto 53 wanaougua maradhi mbalimbali ya moyo wanaondoka nchini leo kwenda India kwa upasuaji ambapo wataagwa na Makamu wa Rais, Dk Ghalib Bilal.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mratibu wa magonjwa ya moyo katika Klabu ya Lions ya Dar es Salaam jana, Dk Rajni Kanabar (pichani), wagonjwa hao watatibiwa katika hospitali mbalimbali nchini India.

Alisema safari ya wagonjwa hao imeratibiwa kwa pamoja na Klabu ya Lions ya Dar es Salaam (Host), Regency Medical Centre na Wizara ya Afya ya Zanzibar.
Alisema katika kundi hilo watakuwamo wauguzi wawili na madaktari wawili na wanatarajiwa kurudi nyumbani ndani ya muda wa wiki nne zijazo.
Dk Kanabar alisema wagonjwa 15 watatibiwa katika Hospitali ya Jaypee Health Care Heart Institute, iliyoko mji wa New Delhi na wengine 27 watatibiwa katika taasisi kubwa ya Fortis Escorts Heart nayo akiwa New Delhi, India .
"Watafanyiwa upasuaji ambao utagharimu dola za Marekani 2,500  kwa kila mgonjwa  na watapewa dola  500 kwa ajili ya kujikimu wakiwa huko ambako watakaa kwa wiki nne," alisema Dk Kanabar ambaye pia ni Mwenyekiti wa Hospitali ya Regency Medical Center.
Alisema hospitali ya Escorts  ni miongoni mwa hospitali kubwa duniani kwa matibabu ya moyo na imekuwa ikiwafanyia upasuaji wagonjwa wa moyo kutoka Tanzania kwa punguzo kubwa la gharama za matibabu hayo.
Aliishukuru Wizara ya Afya ya Zanzibar kwa kuchangia nauli za ndege kwa wagonjwa 33  na kutoa dola 500 (Sh 850,00) kwa kila mgonjwa na Ubalozi wa India ambao viza za bure kwa wagonjwa wote kupitia Balozi wa nchi hiyo nchini, Debnath Shaw.

No comments: