LOWASSA APONGEZA AMANI KISIWANI ZANZIBAR

Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa amewapongeza Wazanzibar na Serikali ya mseto visiwani humo kwa kudumisha amani.
Akitoa salamu zake Krismasi katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT),  Mwanakwerekwe mjini Unguja alikokwenda kusali, Lowassa (pichani) ambaye ni Mbunge wa Monduli mkoani Arusha, alisema hali ya amani visiwani humo sasa ni shwari kabisa.

"Mara ya mwisho wakati niliposali hapa huko nje kulitanda askari Polisi..hali haikuwa shwari, lakini leo hali ni tofauti kuko shwari kabisa," alisema Lowassa na kushangiliwa na waumini waliohudhuria.
Alisema Zanzibar imefanikiwa kushinda changamoto za kuhatarisha amani, na kuiepusha kutumbukia katika hali kama inayojitokeza katika nchi nyingine zikiwemo Nigeria na Kenya.
"Nawaomba ndugu zangu Wazanzibar tuitunze amani hii ili ilete ajira..tuitunze amani ili tupate baraka za Mungu..na wale wenye kutaka kuvuruga amani hii washindwe!" alisisitiza Lowassa.
"Hayati Mwalimu Nyerere aliwahi kusema...mtu akikuuliza kifedhuli Tanzania mna nini mjibu kwa jeuri..tuna amani..na hapa nyinyi mtu akikuuliza kifedhuli Zanzibar mna nini mjibu kwa jeuri: ‘Tuna amani’," alisema.
Aidha, aliungana na Wazanzibari kulalamikia dhana ya mataifa ya Ulaya ya kwamba hata mataifa ya Afrika Mashariki yamekumbwa na ugonjwa wa ebola. 
"Kumekuwa na maneno huko nje kwamba ebola pia huku ipo, hii ni mbaya sana wanatuharibia, hakuna ugonjwa huo wala nini..Zanzibar ni salama atakaye aje," alisema na kushangiliwa.
Kwa muda mrefu sasa umekuwa ni utamaduni wa Lowassa kusherehekea sikukuu ya Krismasi visiwani Zanzibar.

No comments: