TBS YAFUNGIA KIWANDA CHA KUZALISHA JUISI ZA U-FRESH

Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limekifunga kwa muda usiojulikana kiwanda cha U-Fresh Food Limited cha Tegeta Dar es Salaam, kwa kuzalisha juisi ya U-Fresh chini ya kwa kiwango cha ubora unaotakiwa.

Aidha, limewaonya wahusika wa kiwanda hicho, ambao ni watu wenye asili ya China, kutothubutu kuendeleza uzalishaji wa juisi hiyo kinyemela baada ya kuzuiwa juzi, kwa sababu watakuwa wametenda kosa jingine linaloweza kusababisha wasiruhusiwe kufanya biashara ya aina hiyo kwa kukosa uaminifu.
Ofisa Viwango Mwandamizi wa TBS, Selemani Banza alisema uzalishaji wa juisi hizo unafanywa katika mazingira machafu kwa kutumia sukari tamu yenye madhara kwa watoto, hivyo haustahili kuachwa uendelee.
Kwa mujibu wa Banza, hadi kufikia uamuzi wa kukifunga kiwanda hicho, shirika hilo lilifuata taratibu zote za kujiridhisha kuwa kinastahili kufungwa, ikiwemo kupima sampuli za juisi hizo kutoka sokoni na kiwandani kwenye, bila wahusika kujua kama zilikuwa zikifanyiwa uchunguzi, hivyo kubaini kwama zilikuwa na asilimia nyingi za vimelea vya wadudu wanaosababisha maradhi mbalimbali.
“Tatizo tuliloliona ni kubwa hivyo jamii haina budi kuelewa na kuacha mara moja kutumia juisi hizi, maabara zetu hazidanganyi na endapo Mtanzania anayetumia juisi hizo angeona wingi wa wadudu waliopo katika juisi hizo asingeruhusu hata watoto wake waziguse,” Banza alisema.
Aliongeza kuwa, pia uongozi wa kiwanda hicho ulidanganya katika taarifa yake kwa shirika kuwa ilikuwa ikituma sukari kutoka Kilombero, jambo ambalo si kweli. “Kwa sababu ya uchafu na matumizi ya sukari isiyofaa tunakifunga kiwanda kuanzia leo (juzi)”.
Naye Mkuu wa Kitengo cha Mahusiano TBS, Roida Andusamile alisema wafanyabiashara wa kiwanda hicho walivuruga uzalishaji wao kwa kukiuka matakwa ya viwango vya ubora baada ya mkataba wao kuongezwa.
“Kwa sababu ufuatiliaji wetu ni wa siri na wa kila wakati, hata kama mzalishaji amepata leseni ya kukidhi viwango leo, tukagundua amebadilisha utaratibu bila mpangilio na kushindwa kuzalisha katika viwango vinavyotakiwa ikiwa ni pamoja na usafi wa bidhaa tunamchukulia hatua ikiwamo kufunga biashara yake kwa mujibu wa Sheria ya Viwango Namba 2 ya mwaka 2009,” alisema Andusamile.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa uongozi wa kiwanda hicho, William Igogo alisema anachofahamu yeye ni kuwa uzalishaji wa juisi yao unaendeshwa ukiwa na baraka zote za TBS kutokana na kuwa na leseni ya ubora.

No comments: