'WALIOMUUA' DK SENGONDO MVUNGI WALETA KIZAZAAZAA KORTINI


Washitakiwa wa kesi ya mauaji ya Mjumbe wa Tume ya Taifa ya Mabadiliko ya Katiba, Dk Edmund Mvungi (pichani), jana waligoma kutoka katika chumba cha mahakama na kukaa kizimbani kwa muda hadi watakapoelezwa jalada la kesi yao lipo wapi.

Tukio hilo  ni la  jana asubuhi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu baada ya Wakili wa Serikali, Peter Njike kudai kesi imekuja kwa ajili ya kutajwa,  lakini jalada bado lipo kwa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP).
Mshitakiwa, Longishu Losingo alidai “Desemba 12 mwaka huu upande wa Jamhuri ulidai jalada lipo kwa DPP  na leo (jana) wanaleta hadithi, tunaomba tuambiwe uhalali wa kesi hii kwa sababu tunateseka” .
Mshitakiwa mwingine, Masunga Makenza alidai shitaka hilo ni la muda mrefu,  pia hawaifahamu sheria, lakini wanahitaji kujua DPP anaweza kukaa na jalada kwa muda gani?
Wakili wa Serikali,  Njike, alidai wamesikia malalamiko hayo, ambayo yanatokana na kuchelewa kukamilika hivyo watafuatilia ili wakamilishe upelelezi mapema. Alisema pia hakuna sheria inayomuongoza DPP kukaa na jalada na kwa muda gani.
Hata hivyo, Longisho ambaye alikuwa mlinzi wa nyumbani kwa Dk Mvungi, alidai wamechoka na hawana ugomvi na mahakama wala magereza, lakini wana ugomvi na upande wa Jamhuri. Alidai kama  Jamhuri imeshindwa kukamilisha upelelezi, warudishwe polisi.
Aidha, Makenza alidai wapo tayari kushitakiwa, lakini kama mashitaka hayo yangekuwa ya kweli, upelelezi ungekuwa umekamilika. Alidai kama upande wa Jamhuri, haujakamilisha upelelezi wawaachie halafu ukikamilika wakamatwe tena,  lakini siyo kudanganywa.
“Kwa hoja zilizotolewa na upande wa Jamhuri leo hatupo tayari kushuka kizimbani hadi tutakapoelezwa jalada letu lipo wapi na tunakaa chini,” alidai Makenza.
Baada ya kutoa kauli hiyo, washitakiwa wote 10, isipokuwa mshitakiwa mmoja ambaye hakufika mahakamani hapo jana, walikaa chini kwenye kizimba cha mahakama, wakisubiri waelezwe hatma ya jalada la kesi yao.
Hakimu Mkazi, Hellen Riwa aliwasihi wasifanye hivyo, bali wakubali kurudi mahabusu kwa kuwa kesi hiyo, imeletwa kwake kwa ajili ya kutajwa na kupangiwa tarehe nyingine.
Aliwataka washitakiwa wawasilishe malalamiko yao kwa Hakimu Mkazi, Waliarwande Lema anayesikiliza kesi hiyo.  Washitakiwa walikubali kuondoka mahakamani hapo huku wakisema Hakimu Lema akirudi watamlalamikia vikali.
Hii siyo mara ya kwanza kwa washitakiwa hao, kufanya matukio mahakamani hapo, Desemba 6 mwaka jana waliiomba mahakama iangalie uwezekamo wa kuwatenganisha gereza kwa sababu wakikaa pamoja wanapigana, na wanaweza kuuana.
Mbali na Losingo na Makenza, washitakiwa wengine ni Chibago Magozi (32), John Mayunga (56), Juma Kangungu (29), Paulo Mdonondo (30), Mianda Mlewa (40) , Zacharia Msese (33) Msigwa Matonya (30)  na Ahmad Kitabu (30).
Wanadaiwa  kuwa Novemba 3 mwaka jana katika eneo la Msakuzi, Kibwegere, walimuua Dk Edmund Sengondo Mvungi kwa kukusudia.

No comments: