MVUA KUBWA DAR MAJANGA, MTOTO ASOMBWA AKIWA AMELALA


Hivi ndivyo hali ilivyokuwa jijini Dar es Salaam baada ya mvua kubwa kunyesha kwa takribani saa mbili mfululizo.
Mvua iliyonyesha jijini Dar es Salaam, imeleta balaa baada ya kuua watu wawili, katika maeneo tofauti ya jiji, likiwemo tukio la mtoto wa miaka minane kufa baada ya kuzidiwa na maji yaliyoingia ndani ya nyumba aliyokuwa amelala.

Kwa mujibu wa taarifa ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura, matukio hayo yalitokea mchana kwenye maeneo mawili tofauti.
Tukio moja ni la Tandale, ambako  mtoto Nasma Ramadhani (8), akiwa amelala ndani ya nyumba yao, maji ya mvua iliyokuwa ikinyesha yaliingia ndani na kumzidi nguvu  kisha kusababisha umauti wake.
Kamanda Wambura alisema mvua iliyonyesha saa 5:00 asubuhi ilinyesha kwa wingi,  hivyo kuleta madhara ya kujaa maji kwenye barabara kadhaa na pia kuleta maafa hayo ya vifo.
Katika tukio la pili, lililotokea Mwananyamala, mvua hiyo ilisababisha kifo cha ajuza, Habiba Mwishehe (80) aliyeangukiwa  kichwani na ukuta wa nyumba yake na kusababisha mauti yake.
Madhara mengine ni maji kujaa kwenye maeneo mbalimbali, ikiwemo eneo la Mikocheni zilipo ofisi za Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) Mkoa wa Kinondoni Kaskazini,  jirani na Hospitali ya TMJ,  hivyo kuleta usumbufu kwa wananchi wa eneo hilo na magari.
Kamanda Wambura alitoa mwito kwa wananchi  kuwa makini na kuchukua tahadhari hususan kwa watoto, ambao hawawezi kujisaidia inapotokea mvua kubwa kama hiyo, yenye kuhatarisha maisha.
“Kuna tabia ya kuwatuma watoto wadogo dukani wakati mvua inanyesha, wazazi na walezi hii sio sawa, wanaweza kukutana na maji mengi yakawazidi nguvu na kupoteza maisha, pia tuwe waangalifu na maeneo ambako maji yanajaa, kwani wanaokatiza wanaweza kuzama,” alisema Wambura.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala jijini humo, Mary Nzuki  alisema hali ni shwari na hakuna tukio lililoripotiwa kwa muda huo. Aliwataka wananchi waishio mabondeni, kuondoka mara moja badala ya kusubiri maafa.
“Nitoe rai kwa wakazi waishio mabondeni, waondoke mara moja wasisubiri kuondolewa, na mvua hizi hazina hodi na hatujui zitanyesha kwa kiasi gani na muda gani, ni vyema wachukue tahadhari kwanza, maeneo hayo sio salama,” alisema Nzuki.
Kwa upande wake, Kamanda wa  Polisi Mkoa wa Temeke, Kihenya Kihenya alisema hakuna tukio la maafa lililoripotiwa hadi muda huo na kuwataka wananchi kuchukua tahadhari hasa kwa kipindi hichi cha mvua.
Mvua hiyo ilileta kizaazaa kwa watumiaji wa vyombo vya usafiri na wakazi wote wa jiji baada ya maji kujaa barabarani na kushindwa kufanya shughuli zao kwa wakati.
Mvua  ilinyesha kwa saa muda wa saa mbili na iliambatana na radi na upepo na kusababisha maeneo ya katikati ya jiji, barabara zake kujaa maji, hali iliyosababisha usafiri kuwa mgumu. Aidha, mvua hiyo ilisababisha wakazi wa jiji kusimamisha biashara zao kwa muda.
Katika Barabara ya Bibi Titi Mohamed kuanzia maeneo ya Mnazi Mmoja, Akiba hadi Posta barabara hizo zilijaa maji, hali iliyosababisha madereva wa magari madogo kushindwa kupita na kuamua kutafuta njia nyingine huku magari ya Usafiri wa Dar es Salaam (UDA) pekee ndio yalimudu adha hizo.
Pia katika maeneo ya Posta kwenye kituo cha mafuta ya Total, karibu na Benki ya CRDB,  kulijaa maji hivyo wafanyabiashara wa kituo hicho kushindwa kutoa huduma ya mafuta kutokana na kutokuwepo kwa magari yanayoingia katika kituo hicho.
Baadhi ya wakazi wa jiji, walijawa na hofu kwamba kutokana na mvua kubwa iliyonyesha, itaweza kusababisha madhara kwa watu waliokataa kuhama mabondeni.
 Katika eneo la Posta Mpya, usafiri ulikuwa wa shida,  hali iliyosababisha watu kujaa kwenye kituo cha daladala kwasababu magari  mengi yalikuwa hayafiki katika kituo hicho.
Baadhi ya watu walilazimika kuvua viatu na kukanyaga maji machafu, yaliyokuwa yanapita barabarani huku wakilalamikia ubovu wa miundombinu na kutokuwepo kwa mifereji.
Kutokana na maji mengi yaliyotuama barabarani hasa katika eneo la Akiba, magari madogo yaliingia maji na kuzima barabarani.
Mwandishi alilishuhudia gari dogo likiwa limepaki karibu na Hoteli ya Holiday Inn huku dereva na abiria wake wakichota maji  kutoka kwenye gari na kuyamwaga nje.

No comments: