Msichana mmoja mkazi wa Mtaa wa Zaire eneo la
Kijenge Kaskazini mkoani Arusha, amelazwa katika Hospitali ya Mkoa ya
Mount Meru chini ya ulinzi mkali wa Polisi baada ya kujizalisha mwenyewe na
kisha kumtumbukiza mtoto wake kwenye ndoo ya maji.
Baba mwenye nyumba ambayo binti huyo
alikuwa amepanga chumba cha kuishi, Reuben Mollel alisema msichana huyo alikuwa anajulikana kama ‘Dada
Pendo,’ na kwamba maisha yake hayakuwa wazi.
“Alipokuja kupanga hapa alidai kuwa
yeye ni mwanafunzi, ila hivi karibuni pia alionekana kuwa
na mimba, hakuna kilichojulikana tena hadi jana, ambapo nyumba
hii ilizingirwa na wanakijiji ambao hatimaye waligundua kitoto kinachodhaniwa
kuwa ni chake, kikiwa kimezamishwa kichwa chini, kwenye ndoo ya
maji,” alisema baba huyo mwenye nyumba.
Taarifa za uwezekano wa kuwepo mtoto
mchanga ndani ya chumba cha Dada Pendo, ziliibuliwa na
mpangaji mwenzake, Mama Martha Lucas,
ambaye alidai kuwa alisikia sauti ya mtoto mchanga akilia usiku
kucha na baadae kutoweka majira ya asubuhi.
“Nilikwenda kumgongea Dada Pendo
chumbani kwake, kutaka kujua hali ya mtoto aliyekuwa analia usiku na kwa kweli
nilishangaa sana, alipojibu kuwa hajui lolote kuhusu mtoto
wala vilio vilivyokuwa vinasikika usiku huo,” alisema Mama
Lucas.
Hata hivyo, jirani huyo aliamua kutoa
taarifa kwa wapangaji wenzake pamoja na wakazi wengine wa
Kimandolu, ambao walimuita Mjumbe wa Mtaa wa Kijenge Kaskazini,
Gabriel Joseph na pamoja walianza msako wa kukitafuta kichanga hicho,
hii ikiwa ni pamoja na kujaribu kuvunja choo cha shimo cha nyumba hiyo,
wakidhani kuwa mtoto alitupiwa humo.
Baada ya juhudi zao kuambulia patupu,
mkazi mmoja wa eneo hilo, Nelson Kweka, alihisi kuwa
pengine chumba cha huyo dada hakikukaguliwa vizuri na ndipo
alipofunua mfuniko wa ndoo ya maji ya plastiki na kumkuta mtoto mdogo wa
kiume akiwa ametumbukizwa humo, na tayari alikuwa ameshakufa.
Hatimaye polisi walipewa taarifa,
lakini mara walipofika kwenye eneo la tukio, walimkuta dada
mtuhumiwa naye akiwa katika hali mbaya kiafya, pengine kutokana
na juhudi za kujizalisha mwenyewe usiku.
Dada Pendo alikimbizwa hospitalini
Mount Meru, huku mtoto wake ukipelekwa kuhifadhiwa katika nyumba ya
maiti hospitalini hapo.
Ofisa Habari wa Polisi mkoani hapa,
Rashid Nchimbi alisema polisi wanasubiri afya ya dada huyo itengemae ili aweze
kulisaidia jeshi hilo katika uchunguzi zaidi.
No comments:
Post a Comment