MAMLAKA HALI YA HEWA YASEMA MSIMU WA MVUA UMEKWISHA

Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA) imesema msimu wa mvua za mwisho wa mwaka unaisha leo, ingawaje bado inatarajiwa kuwa na mvua kuanzia mapema mwaka 2015.  
Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk Agnes Kijazi alisema hayo Dar es Salaam wakati akizungumzia mvua iliyonyesha juzi na kusababisha athari mbalimbali katika baadhi ya maeneo. 
Akizungumzia mvua hiyo, Dk Kijazi alisema ingawaje bado kuna mvua, lakini msimu wa mvua ulioanza Oktoba, Novemba na Desemba unamalizika leo. 
Alisema msimu huo, mvua haikunyesha kwa kiwango kikubwa zaidi ya ile iliyonyesha juzi  kwa saa mbili katika jiji la Dar es Salaam.
Alisema kuwa mvua zinazotarajiwa kuanza mwanzoni mwa Januari mwaka 2015, itakuwa nje ya msimu na inaweza kuwemo  mvua kubwa pia.
Alisema mvua kwa mwezi wa Januari itanyesha kwa wiki mbili na kuwataka wakulima kujiandaa kwa mazao, ambayo yataweza kupandwa kwa kipindi hicho. Aliwataka wananchi kuwa na tabia ya kufuatilia taarifa za mamlaka hiyo.
Mvua iliyonyesha juzi Dar es Salaam ilileta athari mbalimbali ikiwa ni pamoja na vifo vya watu wawili katika maeneo tofauti huku barabara zikijaa maji na kusababisha watu kushindwa kufanya kazi zao kwa wakati.
Hata hivyo, wakizungumzia athari zaidi kwa mvua hiyo kwa nyakati tofauti, makamanda wa Polisi  wa Mikoa ya  Kipolisi ya  Ilala, Temeke na Kinondoni walisema hadi jana hali ilikuwa shwari na hakuna athari nyingine zilizoripotiwa kutokea.

No comments: