Hakimu Mkazi wa Mahakama ya
Hakimu Mkazi Kisutu, Hellen Riwa amejitoa kusikiliza kesi ya ugaidi
inayomkabili kiongozi wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu
Zanzibar (Jumiki), Shekhe Farid Hadi Ahmed na wenzake.
Hakimu Hellen alitangaza kujitoa kusikiliza kesi
hiyo jana kutokana na uamuzi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam ulioamuru
Mahakama ya Kisutu kusikiliza na kutolea uamuzi ombi, lililowasilishwa na
Shekhe Farid na wenzake.
Akitangaza kujitoa jana Hakimu Hellen alisema:
“Mahakama Kuu ndiyo ina uwezo wa kusikiliza kesi hii…kwa kuwa Mheshimiwa Jaji
ni mkubwa, mimi binafsi siwezi, najitoa”.
Katika ombi lao, washitakiwa waliomba Mahakama
ya Kisutu ifute mashitaka ya ugaidi dhidi yao, pia walihoji uhalali wa
kushitakiwa Tanzania Bara wakati Zanzibar ni nchi ambayo ina Mahakama Kuu na
kuomba wakashitakiwe katika sehemu walizokamatwa.
Hakimu Hellen alisema kwa mujibu wa sheria,
ushahidi hautoki hewani, unatoka kwenye hati ya mashitaka na kwa maoni yake
maelezo ya kesi yalikuwa sahihi, lakini alikuwa anashangaa kwanini washitakiwa
waliletwa Tanzania Bara.
Hata hivyo, alisema baada ya kusoma Sheria ya
Ugaidi aligundua wanaweza kushitakiwa sehemu yoyote na hati ya mashitaka
imeeleza wazi kuwa wanadaiwa kufanya matukio katika maeneo ya Tanzania Bara.
Awali kabla Hakimu hajajitoa, upande wa Jamhuri
ulidai hawakuridhika na uamuzi wa Mahakama Kuu na wameshawasilisha kusudio la
kukata rufaa ili Mahakama ya Rufaa itoe ufafanuzi wa uamuzi huo lakini kwa sasa
wapo tayari kutekeleza kilichoamuliwa.
Upande wa utetezi ulidai Mahakama imeelekezwa
kutoa uamuzi wa hoja zilizotolewa Oktoba 19 mwaka huu na wakaomba hakimu ajitoe
ili Hakimu mwingine asikilize hoja hizo kwa kuwa hakimu Hellen alishatoa
uamuzi.
Hata hivyo, Wakili Kongola alidai hakuna sababu
za msingi za hakimu kujitoa na kama ikiwa ni hivyo, watamaliza mahakimu wote wa
mahakama hiyo.
No comments:
Post a Comment