MWANAFUNZI AJIZOLEA MILIONI 3/- ZA BIMA KUTOKA BAYPORT

Taasisi ya kifedha inayojihusisha na utoaji wa mikopo ya Bayport Tanzania, imempatia Sh milioni tatu mwanafunzi wa mwaka wa kwanza wa Chuo Kikuu kishiriki cha Mkwawa (MUCE), Kennedy Kaupenda, kufuatia huduma mpya ya Bima ya Elimu inayoendeshwa na taasisi hiyo nchini.
Huduma hiyo mpya ya Bima ya Elimu ya Bayport Tanzania ilianza mapema mwaka huu kwa ajili ya kuwapatia fursa wanafunzi kuendelea na masomo baada ya mzazi aliyejiunga na huduma hiyo kufariki dunia.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mratibu wa Bima ya Elimu inayotolewa na Bayport Tanzania, Ruth Bura alisema, Kaupenda alitajwa kama mnufaika kwa mzazi wake aliyefariki dunia, hivyo waliamua kumtafuta kwa ajili ya kumpatia mafao yake.
Alisema huduma hiyo ina vipengele vinne ambavyo ni Bronze, Gold, Silver na Exucutive ambapo  makato ya kila mwezi ya Bronze ni Sh 2,500 huku fao lake likiwa ni Sh milioni 3, wakati makato ya Gold ni Sh 6,250 huku fao lake likiwa ni Sh 7,500,000.
Bura alisema kipengele cha Silver makato yake kwa mwezi ni Sh 3,800 huku mteja akilipwa fao la Sh milioni 4,500,000 na kipengele cha Executive kikihusisha makato ya Sh 9,000 na kumpatia mteja fao la Sh 10,800,000.
“Tunaamini kuwa huduma hii ni sehemu ya kuhakikisha kuwa Watanzania wanawawekea ulinzi wa elimu watoto wao na yeyote wanayemchagua wao ili hata wanapoachwa waweze kunufaika na elimu bila vipingamizi,” alisema.
Akizungumzia fao hilo, Kaupenda alisema hakuwa na imani kuwa angesoma vizuri baada ya baba yake kufariki, ila baada ya kutafutwa na Bayport na kutaarifiwa juu ya mafao hayo, amepata nguvu mpya.
“Nasikitika sana baba kwa kunificha juu ya kujiunga na huduma hii sambamba na kuwa mkopaji wa Bayport, hata hivyo namshukuru kwa sababu fedha hizi zimekuja kunipa mwanga mpya wa kuhakikisha kuwa nasoma kwa bidii, nikiamini kiasi cha Sh milioni tatu kitaniweka katika wakati mzuri mno,” alisema Kaupenda.
Mbali na huduma hiyo ya Bima ya Elimu kwa uwapendao, pia Bayport inajihusisha na mikopo kwa watumishi wa umma na kampuni zilizoidhinishwa, ambapo hivi karibuni walizindua huduma ya Mikopo ya Bidhaa, ambapo bidhaa za bodaboda aina ya Lifan, Toyo na Boxer zinakopeshwa kwa wateja wa Bayport Tanzania.

No comments: