Hali ya usalama katika jiji la Dar es Salaam
imeelezwa kuwa shwari katika sikukuu ya Krismasi huku ulinzi ukiimarishwa zaidi
kuelekea mwisho wa mwaka.
Jiji hilo lenye mikoa mitatu ya Kipolisi ya Ilala, Kinondoni na Temeke,
hakuna matukio makubwa yaliyojitokeza.
Wakizungumza na mwandishi, makamanda wa mikoa hiyo walisema kwa jumla
hali ya usama ni shwari. Walisema licha ya watu wengi kujitokeza katika maeneo
mbalimbali ya starehe, polisi waliweza
kudhibiti usalama.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Mary Nzuki alisema katika mkoa wake
hali ilikuwa ni shwari kwa kuwa polisi walikuwa ni wengi kuhakikisha hakuna
jambo baya linaloweza kutokea.
Alisema, usalama wa kutosha katika eneo lake, unatokana na wao kujipanga
vizuri ili kuhakikisha watu wanasherehekea Krismasi kwa amani.
Aidha, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura alisema
kuna baadhi ya matukio madogo ya kawaida ambayo yalijitokeza lakini
yalidhibitiwa.
Alisema matukio hayo, hayakusababisha uvunjifu wa amani au madhara mengine yoyote.
"Hakuna taarifa zozote za matukio makubwa hata ajali ni magari kwa
magari lakini hakuna ambayo imesababisha kifo, hali ya usalama ni ya hali ya
juu sana na hii itaendelea mpaka kwenye sikukuu za mwaka mpya," alisema.
Alisema ufukwe wa Coco ndiyo huongoza kwa kujaa watu wengi na ndivyo
ilivyotokea, lakini askari pia walikuwa
ni wengi na hakuna tukio lolote
lililojitokeza.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Kihenya Kihenya alisema licha ya kuwa
na kumbi nyingi za starehe, zilizokuwa zikipiga muziki na watu kujaa, hakuna
taarifa za matukio ya uhalifu au ya vifo yaliyojitokeza.
Makanda hao walisema kuwa hali ya usalama itaendelea kuimarishwa katika
kipindi chote na hasa kwa kuzingatia bado kuna sikukuu za Mwaka Mpya.
No comments:
Post a Comment